WAKATI kocha mkuu wa Simba SC, Steve Barker, akiwasisitiza viongozi wa klabu hiyo kuingia sokoni kusaka beki wa kuimarisha safu ya ulinzi, tayari uongozi huo umefanikiwa kukamilisha usajili wa beki Nickson Kibabage kutoka Singida Black Stars.
Hatua ya kumsajili Kibabage inalenga kuongeza nguvu na ushindani ndani ya kikosi cha Simba, hasa ikizingatiwa changamoto za michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara yanayohitaji kikosi imara na chenye kina.
Imeelezwa kuwa Kibabage ni sehemu ya mpango mpana wa maboresho ya kikosi cha Simba, ambapo anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanne ambao tayari klabu hiyo imekamilisha makubaliano nao katika dirisha hili la usajili.
Akizungumza kuhusiana na suala hilo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa kwa sasa hawezi kuweka wazi majina ya wachezaji waliokamilisha usajili, lakini amethibitisha kuwa klabu tayari imefikia makubaliano na nyota wanne.
“Wachezaji wanne tumemalizana nao na tunasubiri muda muafaka wa kuanza kuwatambulisha. Ndani ya muda mfupi utaanza kuona utambulisho wao mmoja baada ya mwingine,” amesema Ahmed Ally.
Ameongeza kuwa baada ya kocha Steve Barker kuwasili na kuanza rasmi majukumu yake kupitia mazoezi na ushiriki wa Kombe la Mapinduzi, alitoa mapendekezo ya maeneo yaliyohitaji kuimarishwa, jambo lililowasukuma viongozi kuingia sokoni na kufanya mazungumzo na wachezaji waliopendekezwa.
“Viongozi waliingia sokoni, wakafanya mazungumzo na wachezaji mbalimbali na hatimaye tumefikia pazuri. Tumefanya maboresho makubwa na mazuri, na tumepata maingizo sahihi yatakayosaidia kuifanya Simba iwe imara zaidi msimu huu,” ameongeza.