UONGOZI wa klabu ya Simba umeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuimarisha kikosi kwa kufikia makubaliano ya awali na kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars Clatous Chama kwa ajili ya kurejea tena ndani ya Msimbazi.
Taarifa zinaeleza kuwa pande hizo mbili zimekubaliana kandarasi ya mwaka mmoja, kinachosalia ni kukamilisha taratibu chache za mwisho kabla ya dili hilo kuwa rasmi.
Chama ni miongoni mwa nyota waliowahi kuacha alama kubwa ndani ya Simba, anaelezwa yupo tayari kwa changamoto mpya baada ya mazungumzo kati yake na uongozi wa klabu kufikia hatua nzuri.
Makubaliano hayo yanaashiria kurejea kwa mchezaji aliyewahi kuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na mchango wake mkubwa katika mafanikio ya timu.
Inaelezwa kuwa taratibu za mwisho za mchezaji huyo zinatarajiwa kukamilishwa leo, ikiwa ni pamoja na kuwasili Dar es Salaam kwa ajili ya kumalizia maelewano binafsi na kisha kutambulishwa rasmi.
Chanzo cha ndani kimeeleza kuwa Simba imepanga kumaliza dili hilo haraka ili kumpata mchezaji huyo mapema ndani ya kikosi.
Uamuzi huo unaonyesha dhamira ya Simba kuhakikisha inapata huduma ya nyota huyo bila kuchelewesha mipango ya benchi la ufundi.
Kwa kurejea kwa Chama, Simba inatarajia kuongeza ubunifu na uzoefu mkubwa katikati ya uwanja, hasa ikizingatiwa ratiba ngumu ya mashindano ya ndani na kimataifa.