KLABU ya Simba SC imemtambulisha rasmi mlinda lango wao mpya, Mahamadou Tanja Kassali, raia wa Niger, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha kikosi chake kuelekea mashindano yajayo ya ndani na kimataifa.
Tanja amejiunga na Wekundu wa Msimbazi akitokea klabu ya AS FAN ya nchini Niger, ambako amekuwa akionesha kiwango kizuri kilichomvutia uongozi wa Simba kumleta nchini Tanzania.
Kupitia taarifa yao kwa umma, uongozi wa Simba umeeleza kuwa kipa huyo ana uzoefu na uwezo mkubwa wa kulinda lango, sifa walizoona zinaendana na mahitaji ya timu katika msimu huu.
Usajili wa Tanja unatajwa kuwa sehemu ya mpango wa Simba kuongeza ushindani katika nafasi ya kipa akichukuwa nafasi ya Moussa Pinpin Camara ambaye bado hajawa fiti, hatua inayolenga kuhakikisha timu inakuwa na chaguo bora na la uhakika kwa kila mchezo.
Mashabiki wa Simba wanatarajiwa kumuona kipa huyo mpya akianza mazoezi na timu mara moja, huku wakitarajia atachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha safu ya ulinzi na kuongeza ushindani ndani ya kikosi.