Home Habari za michezo KUELEKEA AFCON 2027….MOTSEPE ATIA NENO MAANDALIZI YA TZ, KENYA NA UGANDA…

KUELEKEA AFCON 2027….MOTSEPE ATIA NENO MAANDALIZI YA TZ, KENYA NA UGANDA…

84
0
Habari za Michezo leo

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amekutana na Rais wa Shirikisho la Kandanda Barani Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe, Jijini Rabat, Morocco. Katika mkutano huo, Waziri Makonda alimkabidhi Dk. Motsepe barua kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Pamoja na barua hiyo, Waziri Makonda, aliyekuwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amemhakikishia Rais wa CAF kuwa Rais Samia yupo tayari kushirikiana kwa karibu na CAF katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kandanda, ikiwemo mashindano mbalimbali.

Makonda pia alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika maandalizi ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 sambamba na Kenya na Uganda, na imedhamiria kuonyesha tofauti kubwa na mashindano yaliyopita. Aidha, aliomba CAF kuangalia kimkakati mipango ya Tanzania ili kuhakikisha mafanikio makubwa yanayotarajiwa yanapatikana.

Kwa upande wake, Dk. Motsepe alimshukuru Rais Samia kwa barua na salamu zake za upendo na ushirikiano kwa CAF, na aliahidi kuwa CAF ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Tanzania kufanikisha maendeleo makubwa katika mpira wa kandanda.

Dk. Motsepe pia alionyesha kuridhishwa na jitihada za Serikali ya Rais Samia, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na mafanikio makubwa ya mashindano ya CHAN 2024, pamoja na maandalizi ya AFCON 2027 yanayoendelea kwa usahihi.

Aidha, CAF itatuma timu ya wataalamu Tanzania kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kukamilisha maandalizi ya AFCON 2027, ambayo yanatarajiwa kushirikisha nchi 28 badala ya 24 kama ilivyokuwa awali.

Dk. Motsepe ameahidi kutembelea Tanzania hivi karibuni ili kujionea maandalizi ya mashindano hayo na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi mbalimbali.