Home Habari za michezo STRAIKA PRISONS ATUA COASTAL

STRAIKA PRISONS ATUA COASTAL

3
0

ALIYEKUWA mshambuliaji wa maafande wa Tanzania Prisons, Abdulkarim Segeja, amekamilisha usajili wa kujiunga na Coastal Union kwa mkataba wa miezi sita utakaomweka ndani ya kikosi hicho cha Wagosi wa Kaya hadi mwisho wa msimu huu.

Nyota huyo aliyejiunga na Prisons katika dirisha dogo la Januari 2023 akitokea Copco ya jijini Mwanza, alisaini mkataba wa miaka miwili, japo mazungumzo ya kuongeza mwingine yaligonga mwamba na kuamua kutafuta changamoto mpya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Segeja alisema amefikia uamuzi wa kujiunga na Coastal Union katika dirisha hili dogo la usajili huku akiamini timu hiyo itampa nafasi zaidi ya kucheza na kuonyesha kipaji tofauti na alikotoka.

“Kuna mambo ambayo awali hayakwenda vizuri na Prisons, baada ya kukaa na menejimenti yangu tukaona tuvunje rasmi mkataba uliobakia ili niangalie changamoto mpya, hivyo ni kweli nimekamilisha taratibu za kujiunga na Coastal Union,” alisema.

Aidha, mshambuliaji huyo alisema licha ya kukaa nje kwa takribani miezi miwili bila ya kucheza mechi za ushindani, lakini bado alikuwa anaendelea na mazoezi binafsi, ambapo kwa hatua aliyopo anaamini atakuwa chachu ya mafanikio ya Coastal Union.

Nyota huyo wakati anajiunga na Prisons alitokea Copco ya jijini Mwanza iliyokuwa inashiriki Ligi ya Championship, ambapo kwa msimu wa 2023-2024, aliifungia mabao manane, huku akicheza timu mbalimbali ikiwemo TRA United zamani Tabora United.

Pia, Mwanaspoti linatambua nyota wengine walio katika mazungumzo ya kujiunga na Coastal Union ni beki wa kati wa Mbuni ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship, Ambokise Mwaipopo, aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea KenGold.

Mbali na Ambokise, Coastal Union inafuatilia pia saini ya aliyekuwa beki wa kulia wa Geita Gold, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji na JKT Tanzania, George Aman Wawa, ili kwenda kuongezea nguvu kikosi hicho katika dirisha hili la usajili.