KLABU ya Al Ahly ya Misri imetangaza rasmi kikosi chake kitakachocheza dhidi ya Yanga ya Tanzania katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi, unaotarajiwa kuchezwa kesho Januari 23 nchini humo.
Orodha hiyo imetolewa na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Marcel Koller, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Katika kikosi hicho, Ahly imejumuisha makipa wake tegemeo akiwemo Mohamed El Shenawy, sambamba na Mostafa Shobeir na Mohamed Seha, hali inayoonyesha benchi la ufundi limejipanga vyema katika eneo la ulinzi wa lango kuelekea mchezo huo mgumu.
Safu ya ulinzi inaongozwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa akiwemo Mohamed Hany, Ahmed Eid, Yasser Ibrahim pamoja na Yassine Meriah, ambao wanatajwa kuwa na jukumu kubwa la kuzuia mashambulizi ya Yanga yenye kasi na ubunifu.
Katika eneo la kiungo, Ahly imesheheni majina makubwa akiwemo Elio Dieng, Ben Romdhane, Marwan Attia, Emam Ashour pamoja na Ahmed Mostafa Zizo, ambao wanategemewa kudhibiti mchezo wa kati na kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.
Upande wa washambuliaji, mabingwa hao wa Afrika wamemsajili na kumjumuisha nyota wao mpya Trezeguet pamoja na Gradisar, Ben Cherki na Marwan Othman, hali inayoashiria nia ya Ahly kucheza soka la kushambulia dhidi ya Yanga.
Mchezo huo unatajwa kuwa wa presha kubwa kwa pande zote mbili, huku Yanga ikihitaji matokeo mazuri ugenini na Ahly ikilenga kuendelea kuthibitisha ubabe wake barani Afrika.