Home Habari za michezo ECUA KUTUA JS KABYLIE KWA MKOPO

ECUA KUTUA JS KABYLIE KWA MKOPO

8
0

KIUNGO wa Yanga, Celestine Ecua yupo mbioni kujiunga na klabu ya JS Kabylie ya Algeria kwa mkataba wa mkopo, huku taarifa zikieleza kuwa pande hizo mbili ziko katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano hayo.

Inaelezwa kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri kati ya Yanga na JS Kabylie kuhusu mkopo wa mwaka mmoja, ambapo kila kitu kimekaa sawa na kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa taratibu za mwisho ili dili hilo liwe rasmi.

Hatua ya JS Kabylie kumfuatilia Ecua inatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuimarisha kikosi chake kuelekea nusu ya pili ya msimu, hususan eneo la kiungo ambalo benchi la ufundi linaamini linahitaji kuongeza nguvu, ubunifu na uimara zaidi.

Ecua amekuwa akivutia macho ya klabu hiyo kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kusambaza pasi sahihi na kuchangia mashambulizi, sifa ambazo zimeifanya JS Kabylie kuona anaweza kuwa chaguo sahihi kwa kikosi chao.

Kwa upande wa Yanga, kumtoa Ecua kwa mkopo kunatajwa kuwa ni mkakati wa kumpa nafasi ya kupata dakika nyingi za kucheza katika ushindani mkubwa wa soka la Afrika Kaskazini, hatua itakayomsaidia kuongeza kiwango chake binafsi pamoja na uzoefu wa kimataifa.

Iwapo makubaliano hayo yatakamilika kama ilivyopangwa, Ecua ataitumikia JS Kabylie kwa msimu mmoja, huku matarajio yakiwa makubwa kuwa ataongeza ubora ndani ya kikosi hicho na kuchangia mafanikio ya klabu hiyo katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.