Home Habari za michezo SIMBA YASALIA NA MPANGO WA NDANI

SIMBA YASALIA NA MPANGO WA NDANI

60
0

MENEJA  wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa klabu hiyo imefunga rasmi usajili wa kimataifa kwa wachezaji wa kigeni na sasa inaendelea na usajili kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ahmed amesema kuwa kutokana na kanuni za mashindano ya kimataifa, wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa kwa sasa hawawezi kutumika kwenye michuano hiyo, bali wanaingizwa kwenye mfumo wa kucheza Ligi Kuu pekee.

Akizungumza kuhusu mwelekeo wa usajili, Ahmed amesema Simba bado inaendelea kusajili wachezaji wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha ndani.

“Baada ya kumtambulisha Oura leo, tunatarajia kumtangaza mchezaji mwingine kwa lengo la kuongeza nguvu katika michezo ya ndani,” amesema.

Ameongeza kuwa Simba imecheza michezo sita pekee ya Ligi Kuu kati ya 30, hali inayomaanisha bado kuna mechi 24 mbele yao. Kwa mujibu wake, ugumu wa ligi hiyo unailazimu klabu kuendelea kuboresha kikosi ili kufikia malengo waliyojiwekea msimu huu.

Ahmed amesisitiza kuwa zoezi la usajili wa kimataifa limeshafungwa kabisa, wachezaji wote wanaosajiliwa kwa sasa wako kwenye mipango maalum ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika hatua nyingine, baada ya Simba kumtambulisha rasmi Alain Anicet Oura, klabu hiyo pia inatarajiwa kumtangaza rasmi kiungo mshambuliaji Iñno Jospin Loemba, ambaye tayari yupo nchini na ameanza mazoezi na kikosi kinachonolewa na kocha mkuu, Steve Barker.