Home Habari za michezo AL AHLY YAIFUATA YANGA ZANZIBAR

AL AHLY YAIFUATA YANGA ZANZIBAR

35
0

KIKOSI cha  timu ya  Al Ahly ya Misri kumesafiri  leo Januari 29 kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuikabili Yanga SC katika mchezo mgumu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Januari 31 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Misri, Al Ahly iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani kwao, kuingia kwenye pambano hili la pili wakihitaji kusaka alama muhimu zitakazowahakikishia nafasi nzuri katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Mabingwa hao wa kihistoria barani Afrika wameamua kusafirisha kikosi kamili, hatua inayoonesha wazi namna wanavyouthamini na kuuchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo unaobeba presha na heshima kwa pande zote mbili.

Al Ahly wanawasili Zanzibar wakiwa na lengo moja tu, kupata matokeo mazuri dhidi ya Yanga. Hata hivyo, Yanga nao wamejipanga vilivyo, wakitarajia kutumia faida ya kucheza nyumbani pamoja na sapoti kubwa ya mashabiki wao kusaka ushindi muhimu.

Kwa upande wa Yanga, huu ni mchezo wa kufa au kupona, kwani ushindi pekee ndio unaoweza kuwapa matumaini ya kuendelea kusaka tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Mashabiki wa soka wanasubiri kwa hamu pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na lenye ushindani mkubwa, huku Zanzibar ikitarajiwa kuwa kitovu cha burudani, msisimko na mvuto mkubwa wa soka la Afrika.