Home Habari za michezo MZIZE KARIBU KURUDI UWANJANI

MZIZE KARIBU KURUDI UWANJANI

34
0

HABARI njema zimeifikia benchi la ufundi, viongozi pamoja na mashabiki wa Yanga SC baada ya mshambuliaji wao, Clement Mzize, kufikia hatua za mwisho za kurejea kwenye kiwango chake kamili cha ushindani.

Mzize, ambaye kwa sasa yupo Visiwani Zanzibar akiwa na kikosi cha Yanga, amekuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu kutokana na majeraha na maumivu yaliyomsumbua.

Hata hivyo, nyota huyo sasa amepona kikamilifu na hana tena changamoto yoyote ya kiafya, hali inayoongeza matumaini mapya ndani ya kikosi hicho.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, kwa sasa benchi la ufundi linaelekeza nguvu zaidi katika kumjenga Mzize kimbinu na kimwili ili kurejesha ubora wake wa kucheza mechi nzima kwa dakika 90 bila changamoto.

Amesema benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu Pedro Goncalves limeweka mkakati wa kumrudisha taratibu uwanjani, ambapo mshambuliaji huyo ataanza kupewa dakika chache za kucheza kabla ya kurejea kikamilifu kwenye kikosi cha kwanza.

“Mkakati huu unalenga kumkinga dhidi ya majeraha ya mara kwa mara na kuhakikisha anarudi akiwa imara zaidi. Tayari ameanza mazoezi pamoja na wachezaji wenzake, jambo linaloongeza matumaini mapya ndani ya kikosi,” amesema  Kamwe.

Urejeo wa Mzize unatarajiwa kuimarisha zaidi safu ya ushambuliaji ya Yanga, hasa ikizingatiwa mchango wake mkubwa ndani ya kikosi na ushindani mzuri uliopo kutokana na uwepo wa washambuliaji wengine.

Mashabiki wa Yanga sasa wanasubiri kwa hamu kumuona Mzize akirejea uwanjani kwa nguvu mpya, akiwa tayari kuendeleza alipoishia na kuisaidia timu yake kupigania mafanikio katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.