Home Habari za michezo BARKER AWEKA MKAKATI KABAMBE DHIDI YA YANGA

BARKER AWEKA MKAKATI KABAMBE DHIDI YA YANGA

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesisitiza kwamba kikosi chake kitaingia kwenye Kariakoo Derby dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, kwa tahadhari makubwa na maandalizi ya kina, akibainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu.

Barker amesema maandalizi ya mchezo huo yataendana na mechi nyingine za kawaida, lakini akakiri kuwa Derby ni mechi ya kipekee inayohitaji umakini wa hali ya juu na mabadiliko ya haraka uwanjani.

“Ni mchezo unaohitaji kila mchezaji kuwa makini, mwenye nidhamu, na kuonyesha jitihada kubwa kila dakika 90,” amesema .

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amefafanua kuwa baada ya mechi ya hivi karibuni, kikosi kitafanya mazoezi ya kurejesha nguvu (recovery) kabla ya kuanza safari mapema kuelekea Zanzibar, hatua itakayowawezesha wachezaji kujiweka sawa kimwili na kiakili kabla ya kucheza Derby.

Akizungumza juu ya mwenendo wa timu yake, Barker amesema ameridhishwa na juhudi za wachezaji uwanjani. “Licha ya kucheza mechi ngumu, bado kuna mambo machache ya kuboresha, hasa katika umaliziaji wa nafasi na umakini wa safu ya ulinzi,” ameongeza.

Kocha huyo alibainisha kwamba morali ya kikosi ipo juu, na kujitolea kwa wachezaji kunatoa matumaini makubwa. “Kama tutaendelea na kasi hii, nina imani tutashinda mechi nyingi zijazo,” amesema.

Derby hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia ndefu na ukubwa wa timu hizo mbili, kila upande ukihitaji ushindi ili kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi. Simba, kwa upande wake, inaonekana kuweka nguvu kubwa katika maandalizi yake, ikilenga kumaliza kazi mapema na kuondoka na pointi tatu muhimu.