MAMBO yanazidi kuleta changamoto kwa mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah, baada ya kuendelea kuwa nje ya kikosi katika kipindi hiki muhimu cha maandalizi ya michezo ya ushindani, ikiwemo mechi ya Kariakoo Derby dhidi ya Yanga.
Hali hii imesababisha sintofahamu kubwa, hasa baada ya Sowah hivi karibuni kuondolewa kambini Dodoma kwa sababu ya utovu wa nidhamu, mara tu baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa michezo mitano na Bodi ya Ligi Tanzania.
Imeelezwa kuwa uamuzi wa kumtolea nje Sowah ulitokana na utovu wa nidhamu uliyoibuka ndani ya kikosi, hali ambayo imesababisha kutojumuishwa kwake kwenye kikosi cha Simba kinachojiandaa kwa mchezo wa Kariakoo Derby utakaochezwa Machi Mosi Visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kwa sasa nyota huyo hayupo kwenye mipango ya timu, na hatma yake ya kusafiri na kikosi kuelekea Zanzibar bado haijafahamika.
“Sababu za mshambuliaji huyo kuwa nje ya timu zitawekwa wazi na uongozi wa klabu mara tu taarifa rasmi itakapotolewa. Sowah tulimtoa kambini na kumrejesha mara baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, siku iliyofuata akaondoka kambini na kurejea Dar es Salaam.
Sijui kama tutakuwa naye Zanzibar. Yupo nje ya kikosi toka juzi; nini sababu, mpaka pale klabu itakapotoa taarifa,” amesema Ahmed.
Kutokuwepo kwa Sowah kunazua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa Simba, hasa katika kipindi hiki ambacho timu inaendelea kujipanga kwa ajili ya michezo mizito, ikiwemo derby dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
Mashabiki wengi sasa wanasubiri kwa hamu kauli rasmi ya uongozi itakayoweka bayana hatma ya mshambuliaji huyo ndani ya kikosi, huku matumaini ya kuona Sowah akishiriki katika mechi hiyo muhimu yakiwa yamechanganyikana na hofu.