UONGOZI wa klabu ya Simba SC umeweka wazi kuwa unatamani kuona sheria na kanuni za soka zikifuatwa kwa haki katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ukisisitiza kuwa matokeo ya timu hiyo yawe yanatokana na uwezo wao uwanjani badala ya kuathiriwa na maamuzi ya nje.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, wakati kikosi cha timu hiyo kikiondoka kuelekea mkoani Singida kwa ajili ya mchezo wao wa ligi dhidi ya Singida Black Stars.
Ahmed amesema Simba inatamani kuona uwazi na usawa katika usimamizi wa michezo ili kuhakikisha kuwa ushindi au matokeo mabaya yanatokana na uwezo wa timu husika, badala ya kuingiliwa na mtu yoyote.
Amesisitiza kuwa haitakuwa sawa kwa mtu yeyote kusababisha matokeo ya mchezo kwa namna yoyote, kuwa Simba ikiwa itapoteza basi iwe ni kutokana na mapungufu yao, ikiwa itashinda iwe ni kwa ubora walioonyesha uwanjani.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani Jumatano, Machi 11, 2026 katika Uwanja wa Airtel Stadium kuwavaa wenyeji wao Singida Black Stars katika mchezo muhimu wa ligi ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
“Natoa rai kwa wanaosimamia kanuni na sheria kuhakikisha haki inatendeka. Simba ikifungwa au kupata sare iwe kwa madhaifu yetu, lakini tukishinda iwe kwa ubora wetu, asiwepo mtu wa kusababisha matokeo hayo,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa mchezo huo ni muhimu kwa timu zote mbili, huku Simba ikiwa na lengo la kuondoka na ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wake pamoja na kuendelea kukusanya pointi muhimu katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi msimu huu.
Kwa sasa kikosi cha Simba kimeanza safari ya michezo mitatu ya ugenini ambapo mbali na Singida Black Stars, pia kitakutana na TRA United pamoja na Pamba Jiji FC, huku malengo makubwa yakiwa ni kusaka alama tisa muhimu zitakazosaidia kuimarisha nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.