Home Habari za michezo SINGIDA ALENGA USHINDI DHIDI YA MBEYA CITY

SINGIDA ALENGA USHINDI DHIDI YA MBEYA CITY

0

BAADA ya kudondosha pointi sita katika mechi mbili Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga na Simba, kocha wa Singida Black Stars, David Ouma amewataka wachezaji wake kusahau matokeo hayo na kuelekeza nguvu katika mchezo dhidi ya Mbeya City.

Ouma alisema licha ya kupoteza michezo hiyo migumu anaamini kikosi chake kilionyesha kiwango kizuri na kilistahili kupata matokeo bora zaidi, hasa katika mchezo dhidi ya Simba.

Kocha huyo alieleza kuwa kwa sasa ni muhimu kwa wachezaji wake kuweka pembeni presha ya matokeo ya nyuma na kuangalia mbele, wakilenga kupata ushindi katika mchezo unaofuata ambao utachezwa katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

“Tumetoka kucheza mechi mbili ngumu sana dhidi ya timu kubwa kwenye ligi. Ni kweli hatukupata matokeo tuliyoyatarajia, lakini wachezaji walipambana na kuonyesha kiwango kizuri uwanjani,” alisema Ouma.

Aliongeza kuwa, kikubwa kwa sasa ni kuhakikisha timu inarejea kwenye njia ya ushindi kwa sababu ligi bado ni ndefu na kila mchezo uliobaki ni muhimu katika kukusanya pointi.

“Tumewaambia wachezaji wasikae sana kwenye huzuni ya matokeo ya nyuma. Sasa tunapaswa kuangalia mchezo unaofuata dhidi ya Mbeya City na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema.

Singida Black Stars ambayo ipo nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 19 imeshuka dimbani mara 13.