Home Habari za michezo FOUNTAIN GATE YAMUWEKA KANDO LAIZER

FOUNTAIN GATE YAMUWEKA KANDO LAIZER

0

IMEELEZWA Fountain Gate imemuweka kando kwa muda kocha wa kikosi hicho, Mohamed Ismail ‘Laizer’ kutokana na mwenendo usioridhisha wa matokeo ya timu hiyo.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya kupoteza mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 3-0 uliochezwa Aprili 3, mwaka huu mkoani Singida na taarifa zinasema kocha huyo aliitwa Arusha kwa mazungumzo na viongozi wa juu wa klabu hiyo.

Fountain haina matokeo mazuri msimu huu na hivi sasa inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 17, ikishinda nne sawa na sare, ikipoteza tisa.

Laizer amekuwa akiiongoza Fountain Gate tangu Septemba 28, 2025 alipoondoka Denis Kitambi.

Akizungumza na Soka la Bongo, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, amesema wito wa kocha huyo ulitolewa mara baada ya mechi dhidi ya Dodoma Jiji.

“Kocha Laizer aliitwa Arusha na wakubwa wa timu, hatujajua kikao kilikuwa na nini zaidi maana alitakiwa kukutana na Mkurugenzi Japhet Makau mwenyewe na wito wake ulikuja mara baada ya mechi yetu ya mwisho dhidi ya Dodoma Jiji.

“Baada ya kuitwa, akatupigia simu kwamba ameambiwa akae pembeni kwa muda na timu mpaka uongozi utakapomjulisha, ametutakia kila la kheri kwenye muda ambao atakuwa nje ya kikosi.

“Kuna taarifa wakubwa wamemwambia kwenye timu kuna kama mgomo wa wachezaji, sasa binafsi sijaiona hiyo hali lakini kwa matokeo ambayo tunayapata inafikirisha kidogo, tusubiri kuona kipi kitaendelea.”

Hivi sasa Fountain Gate inakabiliwa na mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 16 bora dhidi ya Azam itakayochezwa Aprili 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Wakati Laizer akiwekwa kando kwa muda huku ikiwa bado haijatolewa taarifa ya kuondolewa moja kwa moja au lini atarudishwa kwenye majukumu yake, msimu huu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara, imeshuhudiwa makocha 13 wakiachana na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo matokeo yasiyoridhisha na kupata dili sehemu nyingine.

Walioachana na timu kwa makubaliano ya pande mbili kwa kile kilichoelezwa ni matokeo yasiyoridhisha ni Dimitar Pantev (Simba), Abdallah Mohamed ‘Bares’ (KMC), Marcio Maximo (KMC), Ally Mohamed Ameir (Coastal Union), Mohamed Muya (Coastal Union), David Ouma (Singida Black Stars), Zedekiah Otieno (Tanzania Prisons), Salum Mayanga (Mashujaa), Romain Folz (Yanga) na Malale Hamsini (Mbeya City).

Kwa upande wa Fadlurahman Davids aliachana na Simba baada ya kupata dili Raja Club Athletic ya Morocco, huku Miguel Gamondi akitua Taifa Stars akitokea Singida Black Stars, wakati Dennis Kitambi akiachana na Fountain Gate alipoamua kujiweka pembeni kwa sababu zake binafsi.