KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amefichua kuwa siri ya ushindi walioupata dhidi ya Pamba Jiji FC ilitokana na mabadiliko ya kimfumo waliyolazimika kuyafanya kulingana na mazingira ya mchezo.
Amesema tofauti ya uwanja, hali ya hewa pamoja na uimara wa wapinzani wao uliwalazimu kubadili mbinu na namna ya kucheza ili kuendana na hali halisi ya mechi hiyo.
Akizungumza baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba, Pedro amesema kikosi chake bado kinaendelea kujengwa hatua kwa hatua, huku kila mazoezi yakitoa nafasi ya kuongeza mbinu mpya, suluhisho tofauti na sura ya kiuchezaji kulingana na mahitaji ya kila mchezo.
Kocha huyo amebainisha kuwa mchezo huo ulikuwa na changamoto tofauti na michezo mingine, hali iliyowalazimu kuingia na mpangilio wa kiufundi usio wa kawaida, ingawa waliendelea kushikilia falsafa yao ya msingi.
“Leo ilikuwa hali tofauti kwa sababu mazingira ya mchezo yalikuwa tofauti. Tunaendelea kuijenga timu na kila mazoezi yanatupa nafasi ya kuongeza mwelekeo mpya na suluhisho ndani ya timu,” amesema Pedro.
Pedro amekiri kuwa walikumbana na changamoto ya aina ya uwanja na mazingira ambayo hayakuwaruhusu kucheza soka lao la pasi za utulivu, hivyo walilazimika kucheza kwa nguvu zaidi na wakati mwingine kutumia mipira mirefu.
Amesema hali ya hewa, ubora wa nyasi pamoja na ushindani wa wapinzani vilifanya mchezo kuwa mgumu, lakini ameridhishwa na kiwango walichoonesha wachezaji wake.
Ameongeza kuwa licha ya kutamani kuona umaliziaji bora zaidi katika baadhi ya nafasi walizozitengeneza, bado anaamini timu yake ilionesha kiwango kizuri katika mazingira hayo magumu.
Mbali na hilo, Pedro aliwapongeza mashabiki wa Yanga, maarufu kama Wananchi, kwa kuendelea kuisapoti timu yao bila kuchoka katika kila mechi.