Home Habari za michezo SOWAH AINGIA MATATANI SIMBA, ASHUSHWA U-20 NA KUTOZWA FAINI

SOWAH AINGIA MATATANI SIMBA, ASHUSHWA U-20 NA KUTOZWA FAINI

0

MSHAMBULIAJI wa Simba, Jonathan Sowah, amechukuliwa hatua za kinidhamu kwa kushushwa kucheza na kufanya mazoezi katika timu ya vijana ya U-20, sambamba na kutozwa faini, kufuatia kubainika kuwa na utovu wa nidhamu.

Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, mchezaji huyo aliripotiwa na benchi la ufundi kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na baadaye kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili kwa uchunguzi zaidi.

Ahmed  amesema kamati hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na Kanda Suleiman Kova, ilimhoji Sowah kuhusu tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Baada ya kusikiliza pande zote na kupitia maelezo yake, kamati ilibaini kuwa mchezaji huyo ana hatia.

“Baada ya uchunguzi kukamilika, imebainika kuwa ni mwenye hatia, hivyo amepewa adhabu ya kulipa faini pamoja na kushushwa kufanya mazoezi na timu ya vijana ya U-20,” amesema Ahmed Ally.

Ameongeza kuwa Sowah atakuwa akifanya mazoezi na timu hiyo ya vijana hadi pale kamati itakaporidhika na mabadiliko ya tabia yake, ndipo atakaporejeshwa kwenye kikosi cha timu ya wakubwa.