KOCHA Mkuu wa Mwenge, Mohamed Said ‘Shuberi’ amesema kinachozifanya timu Zanzibar zionekane dhaifu zinapokutana na za Tanzania Bara ni maandalizi mabovu yanayofanywa.
Amesema, kuna tabia ambayo imejengwa ya kuziandaa timu wiki mbili kabla ya mashindano jambo ambalo ni tofauti na Bara ambazo zinatumia muda mwingi kujiandaa.
“Timu zetu zinaonekana kuwa dhaifu zinapocheza na timu za Tanzania Bara kwa sababu zina kawaida za kutojiandaa vizuri, hili halikubaliki kwenye mpira,” amesema.
Amesisita kuwa, mpira sio barafu kama ukiweka maji yanaganda kwa dakika kadhaa, bali kila kitu kinahitaji maandalizi mazuri ili timu iwe bora.
Amesema, kocha hawezi kutumia dakika 3,000 kwa wiki mbili kuiandaa timu ikawa bora, hilo hakubaliani nalo kwani muda huo huwezi kupata mchezaji wa kukupa unachohitaji.
Kocha huyo amesema mchezaji anajengwa na mazoezi na sio kitu kingine, hivyo Zanzibar wapo wachezaji wazuri wenye kuhimili mikiki ya ligi zote lakini wan akosa kuandaliwa.
Akitolea mfano, timu nne za Zanzibar zilizoshiriki Kombe la Muungano msimu wa 2026 ambazo ni KVZ, Mafunzo, Muembe Makumbi na Mlandege, moja pekee ambayo ni Mlandege ndio iliyofuzu hatua ya nusu fainali, hali inayodhihirisha hazikuwa na maandalizi mazuri, hata hivyo, Mlandege nayo imeshindwa kufuzu fainali ikifungwa 3-0 na Simba.
Kocha huyo alibainisha kwamba, timu za Zanzibar zinategemea zaidi mazoezi ya uwanjani, wakati katika kumuandaa mchezaji kuna mazoezi mengine ya ziada kama gym ili kumjenga kimwili ambayo kwa hapa hayafanyiki.






