MAKAMANDA wa Mashujaa na JKT Tanzania, wamejikuta wakipiga hesabu moja msimu ujao za kuwania saini ya kiungo mkabaji Jonas Mkude.
Mkude ambaye amewahi kuzichezea Simba na Yanga kwa kiwango bora, msimu huu hana timu ya kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kuachana na Yanga ulipomalizika msimu wa 2024-2025.
Hivi karibuni, kiungo huyo alitangaza rasmi kwamba msimu ujao 2026-2027 atarejea kusakata kabumbu kwa timu ambayo atafikia makubaliano nayo ya kimkataba.
Taarifa za ndani zililieleza Mwanaspoti kuwa, timu hizo mbili zilishaanza kumuwinda Mkude tangu dirisha dogo la usajili Januari 2026, lakini sasa zimeongeza nguvu katika harakati zao baada ya mchezaji huyo kuweka wazi dhamira yake ya kurejea uwanjani msimu ujao.
Chanzo kutoka ndani kimeeleza kuwa, kila klabu imeanza kufanya hesabu zake kuhakikisha inampata kiungo huyo mwenye uzoefu mkubwa, ambaye anaonekana kuwa na uwezo wa kuongeza uimara katikati ya uwanja.
“Mashujaa na JKT wote walimtaka hata dirisha lililopita, lakini sasa kila mmoja anapanga namna ya kumpata kutokana na Mkude kutangaza kurudi uwanjani, wote wanachopambania kwa Mkude ni uzoefu alionao licha ya uwepo wa mastaa wengine wanaofanya vyema kwenye timu hizo.”
Katika hatua nyingine, Mashujaa FC imeelezwa kumuweka kwenye rada kiungo mshambuliaji, Jamal Saleh, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Mlandege kwa mkopo akitokea Azam FC.
Inaelezwa kuwa Mashujaa wanahitaji kuongeza ubunifu zaidi kwenye safu yao ya kiungo, jambo linalowafanya kumtazama kwa karibu mchezaji huyo anayefanya vizuri katika majukumu ya kutengeneza nafasi.
“Mashujaa wanamtaka Jamal Saleh kwa ajili ya kuongeza ubunifu, hasa kutokana na kiwango anachoonyesha akiwa kwa mkopo Mlandege, viongozi wanaona kuna kitu anaweza kukifanya msimu ujao kwenye timu yao.”