Habari za michezo

FEI TOTO AWAACHA DUBE, CHAMA KWENYE PRESHA YA MABAO

Vardo May 15, 2026 4:24 pm

KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amesema hana presha yoyote wala ushindani binafsi katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akieleza kuwa akili yake yote ipo katika kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri.

Fei Toto ambaye ameendelea kuwa katika kiwango bora msimu huu, anaongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao 11.

Nyuma yake yupo Prince Dube wa Yanga SC mwenye mabao tisa, huku Clatous Chama na Selemani Mwalimu wa Simba SC pamoja na Fabrice Ngoy wa Namungo FC wakifunga mabao manane kila mmoja.

Pia wachezaji wengine wanaoendelea kufanya vizuri katika mbio hizo ni Allan Okello, Pacome Zouzou na Mudathiri ambao wote wamefumania nyavu mara saba huku ushindani wa ufungaji bora ukiendelea kupamba moto kadri msimu unavyokaribia kuhitimishwa.

Akizungumza kuhusu mbio hizo, Fei Toto amesema hafikirii kushindana na mchezaji yeyote binafsi, bali anapambana kuhakikisha timu yake inapata ushindi katika kila mchezo wanaocheza.

“Sishindani na mtu kwenye ufungaji bora, napambana kuisaidia timu yangu kupata matokeo mazuri. Nikiona nafasi ya kufunga ipo na nina uwezo wa kufanya hivyo, nafanya,” amesema Fei Toto.

Nyota huyo ameweka wazi kuwa kwake jambo muhimu zaidi ni kuona Azam FC inapanda kwenye msimamo wa ligi na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali badala ya kujikita kwenye mafanikio binafsi ya kufunga mabao mengi.

Amesisitiza kuwa mabao ni sehemu ya mchezo, lakini mafanikio ya timu ndiyo yenye thamani kubwa zaidi kwake, akiamini ushindi wa pamoja ndiyo furaha kubwa kwa mchezaji kuliko rekodi binafsi.

KOCHA WA RS BERKANE ATUA KWENYE HESABU ZA YANGA YANGA SC, NDOTO YA MIAKA 90 YAKARIBIA KUTIMIA UWANJA BINAFSI WAANZA KUOTA JUA