Habari za michezo

YANGA SC, NDOTO YA MIAKA 90 YAKARIBIA KUTIMIA UWANJA BINAFSI WAANZA KUOTA JUA

Vardo May 15, 2026 4:32 pm

KWA takribani miaka 90 sasa, klabu ya Young Africans S.C. imebeba ndoto kubwa ya muda mrefu ya kumiliki uwanja wake binafsi ndoto ambayo kwa sasa imeanza kugeuka kuwa uhalisia baada ya hatua kubwa za kiuwekezaji na kiutawala kuchukuliwa.

Rais wa klabu hiyo, Hersi Ally Said, amesema historia ya Yanga imejengwa juu ya msingi wa uzalendo, kujitolea na maono ya viongozi waliotangulia ambao walihakikisha klabu inabaki na utambulisho wake imara kwa miaka yote hiyo.

Hersi amesema juhudi za viongozi wa zamani ndizo zilizozaa matunda ya sasa, kwani ndizo zilizosaidia klabu hiyo kumiliki eneo la ardhi lenye ukubwa wa mita za mraba 35,000. Ardhi hiyo, ambayo imehifadhiwa kwa zaidi ya nusu karne, sasa ndiyo msingi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa unaotarajiwa kubadilisha historia ya klabu hiyo.

Akizungumzia safari ya uongozi wake, Hersi amebainisha kuwa mojawapo ya malengo yake makuu alipoingia madarakani ilikuwa ni kuhakikisha Yanga inapata uwanja wake binafsi. Hata hivyo, amesema alitambua kuwa mafanikio ya uwanjani yalikuwa muhimu kwanza ili kuongeza thamani ya klabu na kuvutia wawekezaji.

Ameongeza kuwa mafanikio ya timu katika mashindano mbalimbali yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mvuto wa klabu hiyo, sambamba na ongezeko la wanachama ndani na nje ya nchi, hali ambayo imefungua milango ya uwekezaji mkubwa.

Katika hatua kubwa ya kihistoria, Hersi ametangaza kuwa Yanga SC imeingia makubaliano ya ubia wa asilimia 50 kwa 50 na GSM Group, ambapo klabu itatoa ardhi huku GSM Group ikichangia mtaji wa kifedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wa kisasa.

Amesema baada ya mchakato wa zabuni na tathmini kukamilika, Kamati Kuu ya klabu iliridhia rasmi GSM Group kuwa mbia mkuu wa mradi huo, hatua inayotarajiwa kuharakisha ujenzi na kuhakikisha uwanja huo unakidhi viwango vya kimataifa.

Hersi amehitimisha kwa kusema kuwa uwanja huo unatarajiwa kukamilika na kuzinduliwa ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi 20 ijayo, akisisitiza kuwa huu ni mwanzo wa ukurasa mpya katika historia ya Yanga SC na ishara ya ukuaji mkubwa wa klabu hiyo ya wananchi.

FEI TOTO AWAACHA DUBE, CHAMA KWENYE PRESHA YA MABAO TOURE AWEKA WAZI, SIMBA SC HAKUNA MZAHA NA MBIO ZA UBINGWA