Habari za michezo

KOCHA WA RS BERKANE ATUA KWENYE HESABU ZA YANGA

Vardo May 15, 2026 4:20 pm

UONGOZI wa Yanga SC unaendelea na mchakato wa kutafuta mrithi wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Pedro, huku jina la kocha kijana kutoka Morocco, Amine El Karma likitajwa kuingia kwenye orodha ya makocha wanaotazamwa kuinoa timu hiyo kuelekea msimu ujao.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa Yanga inamfuatilia kwa karibu kocha huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye aliwahi kuifundisha RS Berkane na kupata mafanikio makubwa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa barani Afrika.

Amine El Karma anatajwa kuwa miongoni mwa makocha wenye falsafa ya soka la kushambulia pamoja na nidhamu kubwa ya kiufundi, jambo linaloonekana kuwavutia viongozi wa Yanga wanaotaka kuendelea kuwa na timu yenye ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

Mashabiki wa Yanga tayari wameanza kutoa maoni yao kufuatia taarifa hizo, ambapo baadhi wanaamini kuwa ujio wa kocha huyo unaweza kuongeza ushindani kutokana na uzoefu wake katika michuano ya CAF pamoja na uwezo wa kusimamia timu zenye presha kubwa ya matokeo.

Hata hivyo, mpaka sasa Yanga bado haijatoa taarifa rasmi kuthibitisha kuanza mazungumzo na Amine El Karma, huku ikielezwa kuwa mchakato wa kusaka kocha mpya unaendelea kwa siri kubwa ili kuhakikisha wanapata chaguo sahihi kwa ajili ya malengo yao ya msimu ujao.

Iwapo dili hilo litakamilika, Yanga inaweza kumpata tena kocha mwenye wasifu mkubwa kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini, eneo ambalo limeendelea kutoa makocha wenye mafanikio makubwa katika soka la Afrika kwa miaka ya karibuni.

HUU SIO MUDA WA KUSHANGILIA HII VITA BADO, AHMED ALLY FEI TOTO AWAACHA DUBE, CHAMA KWENYE PRESHA YA MABAO