Habari za michezo
BARKER AWALENGA VIJANA SIMBA, AFUNGUA MILANGO YA HISTORIA MPYA MSIMBAZI
Vardo
May 18, 2026
8:22 pm
KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi kuwa klabu hiyo inaendelea kuwekeza kwa makusudi katika kuwapa nafasi wachezaji chipukizi ili kujenga kikosi imara kitakachodumu kwa miaka ijayo.
Barker amesema hatua ya kuwapandisha wachezaji wawili kutoka timu za vijana, Hussein Mbegu na Bashiri Kibaila, ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuimarisha safu ya kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi.
Katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA United, Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0, lakini macho mengi yalivutiwa zaidi na mchango wa vijana hao waliopata nafasi ya kucheza.
Kibaila alifanikiwa kuandika jina lake kwenye ubao wa mabao baada ya kufunga bao la nne la Simba, tukio lililozidi kuonyesha kuwa vijana hao wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa timu hata kwenye mechi za ushindani mkubwa.
Akizungumzia bao hilo, Barker amesema halikuwa bao la kawaida kwenye matokeo tu, bali lilikuwa uthibitisho wa juhudi, nidhamu na uwezo wa mchezaji kijana anayepambana kutafuta nafasi yake ndani ya kikosi.
Kocha huyo aliongeza kuwa ana furaha kuona vijana kama Mbegu na Kibaila wakionyesha ujasiri mkubwa uwanjani, akisisitiza kuwa hilo ni jambo muhimu kwa mustakabali wa Simba na hata timu ya taifa kwa ujumla.
Barker amesema ushindi huo wa 4-0 unawapa Simba morali kubwa kuelekea mechi zijazo, kuwa Kibaila ameonyesha njaa, ari na ubora unaoweza kumfanya kuwa sehemu muhimu ya kikosi endapo ataendelea kujituma zaidi.