Habari za michezo
YANGA YAMUWEKA MTEGONI MWAMNYETO, HATMA YAKE YAANZA KUIBUA TAHARUKI
Vardo
May 21, 2026
8:29 am
UONGOZI wa Yanga SC umeanza kuweka mezani hatma ya nahodha wake, Bakari Mwamnyeto, huku sintofahamu kuhusu mkataba mpya wa beki huyo ikiendelea kuzua mjadala mkubwa ndani na nje ya klabu hiyo.
Mwamnyeto ambaye amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu, lakini hadi sasa hakuna mazungumzo rasmi yaliyoanza kati yake na uongozi wa Yanga kuhusu kuongeza mkataba mpya.
Ukosefu wa taarifa za wazi kutoka ndani ya klabu umeongeza presha kwa mashabiki na wanachama wa Yanga, ambao wameanza kuhoji mustakabali wa nahodha huyo ndani ya kikosi, hasa ukizingatia mchango wake mkubwa katika mafanikio ya timu hiyo misimu ya karibuni.
Baadhi ya wadau wa soka wanasema ukimya huo unaweza kuwa ishara ya mipango mipya inayofanywa na klabu hiyo kuelekea msimu ujao, ingawa bado hakuna uthibitisho rasmi unaoonyesha Yanga imeamua kumtema beki huyo au la.
“Kwa sasa hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika, lakini hilo halimaanishi kwamba klabu imeamua kuachana naye. Huenda maamuzi yakafanyika baada ya msimu kumalizika,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Yanga imeanza kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho kwenye safu yake ya ulinzi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani ndani ya kikosi kuelekea msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Majina ya mabeki kama Nasri Kombo wa TRA United pamoja na Mohamed Mussa wa Mashujaa FC yameanza kuhusishwa kwenye mipango ya uongozi wa Yanga, kutokana na kiwango chao kizuri kilichoibua macho ya vilabu vikubwa nchini.
Hadi sasa klabu ya Yanga haijatoa tamko rasmi kuhusu hatma ya Mwamnyeto wala mipango yoyote ya usajili wa mabeki wapya, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu hatma ya nahodha huyo ambaye ameendelea kubeba jukumu kubwa la uongozi ndani ya kikosi hicho.