CHAMA MAJERUHI SIMBA SC YAWEKA WAZI HALI HALISI
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Simba SC Ahmed Ally, amefafanua hali ya kiungo mshambuliaji Clatous Chama, akibainisha kuwa mchezaji huyo hana majeraha makubwa kama ilivyodhaniwa na baadhi ya mashabiki.
Ahmed amesema Chama alionekana kuwa na uchovu wa kawaida uliotokana na ratiba nzito ya mechi mfululizo, hali ambayo ni ya kawaida kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano yenye ushindani mkubwa.
Ameeleza kuwa baada ya michezo, wachezaji hupatiwa huduma za kitabibu mara moja, ikiwemo kuwekwa kwenye barafu ili kupunguza maumivu ya misuli na kusaidia kuharakisha urejeaji wa mwili katika hali yake ya kawaida.
Kwa mujibu wa Ahmed, hatua hiyo ni sehemu ya kawaida ya maandalizi ya kisasa ya michezo na haipaswi kuchukuliwa kama ishara ya jeraha kubwa au tatizo linalohitaji hofu kwa mashabiki.
“Chama yupo mzima na salama, kile kuchechemea kulitokana na uchovu wa mchezo. Ndiyo maana mchezaji akimaliza mechi huwekwa kwenye barafu ili kupunguza maumivu ya misuli,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa hali kama hiyo huwakumba wachezaji wengi hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu ambacho huwa kigumu kimwili na kiakili kutokana na ushindani uliopo.
Ahmed ameongeza kuwa Chama kwa sasa yupo mapumziko mafupi, na anatarajiwa kurejea mazoezini Jumatatu ya Juni Mosi akiwa fiti na tayari kuungana na wenzake katika maandalizi ya michezo ijayo.