ENGLAND KUTUMIA AI KUPIGA PENALTY KOMBE LA DUNIA
LONDON, ENGLAND: Timu ya taifa ya England katika kuhakikisha inafanya vizuri katika Kombe la Dunia imeweka nguvu kubwa katika matumizi ya akili mnemba(AI) kuanzia upigaji wa penalti, kufuatilia ustawi wa wachezaji hadi kubaini udhaifu wa kimkakati wa wapinzani wao.
Teknolojia ambayo inaanza kubadilisha dunia inayotuzunguka inaweza kweli kuisaidia England kupata mafanikio huko Marekani, Canada na Mexico.
Mbali na makocha na wataalamu wa tiba wanaokaa pamoja na kocha mkuu Thomas Tuchel kwenye benchi, wafanyakazi wa England pia wanajumuisha makundi ya wachambuzi, wanasayansi wa takwimu na timu za ndani za watengenezaji wa programu.
Wanatumia zana mbalimbali za AI, baadhi zimenunuliwa kutoka kampuni za teknolojia za nje na nyingine zimetengenezwa ndani ya The Football Association — kuchambua takwimu, kupata taarifa muhimu na kuandaa mawasilisho yanayotumika kwenye mikutano ili kufanya taarifa ngumu kueleweka kwa makocha na wachezaji.
Lengo ni kuhakikisha wachezaji wa England wana uwezo wa kufanya uamuzi bora zaidi uwanjani, ikiwemo namna ya kupiga penalti.
“AI inaweza kuonyesha tabia fulani za wachezaji wa timu pinzani kuhusu wanapoweka penalti zao ambazo huenda hatukuwahi kuzifikiria,” anaeleza Rhys Long, ambaye tangu mwaka 2016 amekuwa mkuu wa uchambuzi wa utendaji na taarifa ndani ya FA.
“Tunapofika kwenye Kombe la Dunia, tunakuwa na taarifa za timu 47 za kuchambua — kila mchezaji katika kila kikosi ameweka wapi penalti zake tangu akiwa na miaka 16?
“Ilikuwa ikituchukua siku tano kukusanya taarifa za penalti za timu moja. Kwa kutumia AI, sasa tunaweza kufanya hivyo ndani ya takribani saa tano. Halafu hiyo hugeuka mazungumzo ya dakika tano na kipa wetu, kwa sekunde tano za matumaini ya kuokoa penalti.”
Kwa hiyo, kinadharia, taarifa za penalti zilizoandikwa kwenye chupa ya maji ya kipa Jordan Pickford sasa ni sahihi na zenye maelezo mengi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Tangu Long ajiunge, rekodi ya England kwenye penalti imeimarika kwa kiasi kikubwa, huku matumizi ya AI na wachambuzi pia yakitumika kupunguza presha ya kisaikolojia kwa wachezaji wa England wanapochagua sehemu ya kupiga penalti zao.
AI NA MAISHA YA WACHEZAJI NJE YA UWANJA
AI haitumiki tu na timu ya taifa ya England kwa masuala ya uwanjani, bali pia kufuatilia afya na ustawi wa wachezaji.
“AI inachofanya ni kuibua mambo muhimu, inaweza kuangalia ni nini kinaathiri mchezaji kimwili, kimkakati au kiufundi,” amesema Rhys Long. “Inaweza kugundua jambo fulani kwenye taarifa za ustawi tunazokusanya kutoka kwa wachezaji ambalo linaweza kuwa linaathiri mazoezi yao.
“Kisha daktari, mtaalamu wa mazoezi ya viungo, kocha au mchambuzi maalum huzungumza na mchezaji kuhakikisha tunapata kiwango bora kutoka kwake.
“Kujaribu kufanya yote hayo haraka zamani kulikuwa kunachukua siku kadhaa. Sasa kunachukua saa chache. Huenda siku zijazo kukachukua dakika chache tu.”
Conor Coady alielezea mchakato huo: “Unaamka kila asubuhi na unapokwenda kupata kifungua kinywa kuna eneo la ustawi ambapo unajaza fomu kwenye iPad.
‘Umelalaje? Umejisikiaje asubuhi hii? Umechoka?’ Halafu unaandika maoni yako, labda ‘misuli ya nyuma ya mapaja inauma kutokana na mazoezi ya jana’.
“Kisha wafanyakazi wanakuhudumia siku nzima kulingana na mahitaji yako mazoezini, chakula, na jinsi wanavyopanga vipindi vya mazoezi.
“Umakini wanaoweka kwa kila mchezaji mmoja mmoja, na muhimu zaidi timu nzima, ni wa kiwango cha ajabu.”