Michezo

KIKAPU PEMBA UMEZIDI KUKUA LICHA YA CHANGAMOTO

Vardo May 27, 2026 6:06 pm

MAENDELEO ya Mpira wa Kikapu Pemba yamekuwa yakiongezeka taratibu miaka ya hivi karibuni ingawaje bado yapo maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa kufikia viwango vya juu.

Licha ya mchezo huo kukabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo kukosa mashindano hasa ya ndani, timu zinapopata nafasi zinaonesha ubora wake.

Soka la Bongo imeshuhudia Ligi Kuu ya Kikapu Zanzibar kufanyika kisiwani hapa iliyochezwa uwanja wa Tennis, Wilaya ya ChakeChake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Mwandishi wa makala hii alipata nafasi ya kukutana na Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Zanzibar, Thani Lali Mfamau ambapo alibainisha mipango ya kukuza vipaji vya mpira kikapu na kuendeleza mashindano ya mchezo huo.

Anasema, maendeleo ya Mpira wa huo kwa upande wa Pemba ni mazuri hasa walipoamua kuwa tayari na kuwajibika kwa kila hatua.

Ameeleza kwamba, Shirikisho hilo linajivunia kwa kuanzisha mashindano ya mpira huo msimu huu wa 2025-2026 kuanzia mwanzo hadi mwisho kwani awali yalikuwa yanaishia njiani bila kumalizika.

Kwa msimu huu wameanzisha Ligi Kuu ya Mpira huo kwa Kanda ya Unguja na Pemba na washindi waliopatikana wamechuana vikali kwenye ligi hiyo iliyochezwa Kisiwani Pemba, ChakeChake.

“Washindi wa Ligi hii kwa wanawake na wanaume watapata nafasi ya kutuwakilisha kitaifa na msimu huu utakuwa umemalizika,” anasema

Anasema, kila mashindano yanayofanyika visiwani hapa ni jukwaa muhimu la kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia utalii wa michezo.

CHANGAMOTO

Kila penye mafanikio hapakosi changamoto na Katibu huyo anaeleza wanayopitia Shirikisho hilo ijapokuwa wanasonga mbele bila kurudi nyuma.

Ametaja changamoto hizo ni pamoja na Shirikisho hilo kukosa ofisi, kukosa kiwanja ambapo hii inawanyima fursa ya kuamua rasmi tarehe ya kuanza mashindano.

Anasema, Laiti wangekuwa na kiwanja chao cha uhakika ingewarahisishia kufanya kazi zao kwa urahisi na ufanisi wa hali ya juu.

Hatahivyo, Katibu huyo ameiomba Serikali kuvizungushia uzio na kuvifunika viwanja vya vikapu ili waweze kuvitumia wakati wa jua na mvua kwani ikitokea mashindano hayo yanaendelea kisha ikanyesha mvua inawabidi wasitishe hadi itakapomalizika.

Amesisitiza, viwanja hivyo vikifunikwa itawarahisishia kupanga mashindano na kumaliza ratiba yao  kwa kuzingatia muda.

“Viwanja vya mpira wa kikapu vilivyojengwa vinakidhi vigezo ila havijafunikwa ikinyesha mvua inatulazimu kusitisha hadi mvua ikimaliza tufute maji ndio tuendelee,” anasema

Vilevile, Katibu Thani ameendelea kusisitiza kwamba Serikali inapojenga viwanja hivyo washirikishe wadau kuwashauri namna viwanja vinavyotakiwa kuepusha gharama mara mbili.

“Natamani tupate viwanja vinne vilivyofunikwa hilo litasaidia mchezo huo kukuza vizuri, hatuwezi kuwasaidia vijana kwa kuwaweka kwenye jua na mvua,” anasema

Mwanaspoti imeshuhudia viwanja kadhaa vya mchezo huo vilivyojengwa ikiwemo kiwanja cha Teniss na Gombani upande wa Pemba, Mao Zedong na Maisara kwa Unguja.

MIPANGO YA KUENDELEZA KIKAPU KWA VIJANA

Akizungumzia suala hilo, anasema Shirikisho hilo kupitia Kamisheni ya michezo ya vijana imepewa dhamana ya kusimamia vijana kuanzia Shule ili kuibua vipaji.

Anaeleza, Shirikisho hilo limejikita kufanya mafunzo kwa timu zinazoshiriki mchezo huo kwa lengo la kuleta ushindani hususani kwa timu zinazotokea kisiwani Pemba.

WADHAMINI WAKARIBISWA KUWEKEZA

Katibu huyo, anasema hakuna mdau yoyote ambaye amejitokeza kuunga mkono mchezo huo hivyo ametoa wito kwao kujitokeza kwa lengo la kuwapa mazingira mazuri vijana hao.

KATIBU ALIA NA BAJETI YA SHIRIKISHO

Thani amesema Shirikisho halina bajeti maalumu kwa maana hiyo linaendesha mashindano yake kwa kutegemea michango ya vilabu vinavyochangia kushiki ligi Kanda ya Unguja na wahisani wenye kuguswa hutoa chochote kitu.

Anasema, Fedha hizo zinazopatikana zinatumika zaidi kuwalipa waamuzi wa mchezo na baadhi ya mambo muhimu yanayohitajika kwenye mashindano hayo.

Katibu Thani anaeleza, kwamba gharama zote zinazotumika kwa mashindano ya Ligi Kanda zote mbili na Ligi Kuu Zanzibar ni Sh35 milioni, kwahivyo Shirikisho pekee yake halina uwezo wa kutoa fedha hizo bila ya kusaidiwa.

Thani anaendelea kuiomba Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni Zanzibar kuwatengea fungu maalumu kwa ajili ya kuendeshea mashindano ya mchezo wa mpira wa kikapu.

TIMU PEMBA KUSHIRIKI MASHINDANO YA KITAIFA

Anasema Pemba imehamasika sana na michezo kwasasa imekuwa na uwezo wa kutoa timu zinazoshiriki mashindano ya kitaifa na hayo ndio maendeleo yenyewe.

Katibu huyo, amesema kinachomkwaza na wakati mwengine kurudisha nyuma ni jiografia ya Pemba, timu inatumia masafa  marefu na gharama kubwa kufuata mashindano yanapofanyika.

Hivyo, anatamani Shirikisho hilo lingekuwa na uwezo wa kuzisaidia gharama timu hizo ili kazi yao kubwa kucheza na sio kugharamika.

Anaongezea kuwa, Shirikisho hilo lina mikakati mipana ya kuendeleza mchezo huo Zanzibar ndio sababu ya kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha unafanikiwa.

Mbali na hilo, Katibu huyo ametoa wito kwa Wizara ya michezo kutenga fungu kwa ajili ya mashirikisho ya vyama vya michezo kuwasaidia kuendesha mashindano kwa uhakika.

WITO KWA VIJANA

Amewasihi vijana kucheza mchezo huo huku wakiwa na matumaini mazuri ya kufikisha mbali na ajira za kusaidia familia zao.

Pia, amewataka wanamichezo kuzidisha nidhamu kwenye mchezo huo kwani ndio jambo la msingi litakalowafaya wafike mbali.

Alisema suala jengine litakalowafanya wafike mbali ni umoja na mashirikiano kwani jambo hilo ndio njia ya mafanikio.

Vilevile, amewasisitiza wachezaji wa mchezo huo kuwa na umoja na mshikamano, vitu hivyo ndio njia ya mafanikio yao wasipuuze.

WADAU WATIA NENO

Wadau wa michezo kisiwani Pemba wamefurahishwa kwa Ligi hiyo kuchezwa hapa huku wakieleza ligi hiyo itaibua muamko wa vijana kwa michezo.

Ame Shaali Ame, amesema ligi hiyo imekuwa fursa kwa vijana kupambana na timu zinazotokea kisiwani hapa kuonesha ushindani.

“Ligi hiyo ilisimama kwa takribani miaka miwili haichezi kisiwani hapa baada kurejea kwa kasi, hatutakiwi kupuuza bali tutoe hamasa kwa vijana,” amesema

Mdau huyo.

Naye, Abrahman Khamis amesema mashindano hayo yamejenga imani kwa vijana kupata mafanikio kupitia mchezo huo.

Amesema, Wanaishukuru Serikali kujenga viwanja vingi vya mchezo huo kisiwani hapa kwani hiyo ni njia mojawapo za kuutambulisha mchezo huo kitaifa.

Mashindano hayo yameshiriksha timu nane ikiwemo nne kutoka kisiwani hapa na Unguja na yanaenda vizuri kwani hakuna anayekubali kushindwa.

Ametoa wito, kwa vijana kushiriki mchezo wa kikapu hususani kwa wanafunzi kwani unaweza kumsaidia mtu kupata scholarship za masomo jambo ambalo linaongeza hadhi na thamani kwa familia.

HITIMISHO

Mpira wa kikapu kisiwani Pemba una mwelekeo mzuri wa kukua lakini unahitaji msukumo wa kifedha na mipango madhubuti ili kufikia mafanikio makubwa.

Kinachohitajika kwenye mchezo huo ni uwekejezaji katika viwanja na vifaa na mafunzo kwa makocha na waamuzi kwa lengo la kuvutia wadhamini.

ENGLAND KUTUMIA AI KUPIGA PENALTY KOMBE LA DUNIA