Ibenge Azam FC
Azam FC

‘ISHU’ YA IBENGE KUWA KOCHA MKUU MALI….MABOSI AZAM FC WAVUNJA UKIMYA…

admin May 27, 2026 9:30 pm

KAMA kuna taarifa inayowasumbua mabosi wa Azam FC na mashabiki wake kwa sasa, basi ni habari inayodai kocha Florent Ibenge anakwenda kuifundisha timu ya taifa ya Mali ambayo anaidakia kipa Djigui Diarra wa Yanga.

Taarifa zinadai kuwa Ibenge alituma maombi ya kuwania kazi ya kuifundisha timu ya taifa ya Mali baada ya shirikisho la soka la nchi hiyo kuachana na Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye aliwahi kuifundisha Yanga miaka ya nyuma.

Taarifa zinaeleza kuwa kocha huyo raia wa DR Congo amefanikiwa kupenya katika hatua ya mwisho ya mchujo wa makocha watano, na kwa sasa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya kuinoa Mali.

Katika mchujo huo, Ibenge amewapiku makocha wengine wanne akiwemo mzawa Mohamed Magassouba, Badou Zaki wa Morocco pamoja na Wareno wawili Antonio Conceicao Oliveira na Antony Da Silva.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mali, mabosi wa shirikisho hilo wanataka Ibenge aanze kazi haraka kwa ajili ya mipango ya timu ya taifa, lakini kocha huyo anataka amalize majukumu yake Azam FC kabla ya kuondoka rasmi mwishoni.

“Florent (Ibenge) hataki kuondoka vibaya Azam FC kwa sababu anaona wamekuwa wakimheshimu tangu alipoanza kazi. Lakini nafasi ya kuifundisha Mali ni kubwa na ina fedha nyingi,” alisema mmoja wa marafiki wa karibu wa kocha huyo.

“Ndiyo maana anataka kuondoka kwa salama baada ya kumaliza mechi za msimu huu akiwa na Azam.”

Jitihada za  kumtafuta kocha huyo kufahamu kuhusu uamuzi wake wa kwenda Mali na kuachana na Azam FC, ziligonga mwamba baada ya simu yake kutokupatikana.

Akizungumzia suala hilo, mkuu wa kitengo cha habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema wanaziona taarika hizo katika mitandao na kocha huyo ana mkataba wa miaka mwaka moja wenye kipingele cha kuongeza mwingine.

“Hizo taarifa hata sisi tunaona kwenye mitandao na nyie waandishi mkipiga simu kutaka kuzungumzia hilo… suala hilo halijafika mezani kwetu. Kocha anatimiza majukumu yake kwenye klabu na sisi viongozi tunatimiza ya kwetu,” alisema Zakazi.

“Tupo katikati ya msimu msisitizo wetu upo kwenye ligi na FA hayo mengine ni mageni. Kocha ana mkataba wa miaka miwili na sisi.”

Mmoja wa viongozi wa Azam ambaye hakutaka kutajwa jina  alisema hawana haraka ya kukamilisha mchakato wa kusaka mrithi wa Ibenge wakiamini akili yake ni kuendelea kuijenga timu hiyo ikiwamo kuanza mipango ya usajili wa msimu ujao.

“Imetushtua kwa kweli. Tulishakaa tukazungumza naye na mpaka tukakubaliana atasaini. Kilichokuwa kimebaki ni kusaini tu mkataba. Hatukuwa na haraka kwa sababu tuliona ni mtu ambaye akili yake ipo Azam FC. Mpaka sasa hajatuambia lolote rasmi, lakini tumejiridhisha kwamba ni kweli aliomba kazi Mali,” alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa Azam haiwezi kumzuia Ibenge ikiwa atapata nafasi hiyo kutokana na mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu.

KIKAPU PEMBA UMEZIDI KUKUA LICHA YA CHANGAMOTO NGOJA KWANZA….MATOLA ‘ANASEPA’ SIMBA NA HUYU NDIYE MRITHI WAKE…?