WALIOCHEZA KOMBE LA DUNIA NA UMRI MDOGO
OHIO, MAREKANI: NI kina nani waliokuwa wachezaji wenye umri mdogo zaidi kuwahi kucheza katika historia ya Kombe la Dunia? Hapa tunaangazia wachezaji 10 wadogo zaidi kuwahi kushiriki michuano hiyo.
Ilikuwa ni katika mchezo kati ya Ireland Kaskazini dhidi ya Yugoslavia uliopigwa Juni 17, 1982 ambapo akiwa kijana mdogo, Norman Whiteside alilinganishwa mara moja na nyota mwingine wa Ireland Kaskazini, George Best, na hata alisajiliwa na Manchester United na mtu yuleyule aliyemuona Best.
Licha ya matatizo ya majeraha yaliyomsaka mapema na hatimaye kufupisha maisha yake ya soka, Whiteside aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza Kombe la Dunia akiwa na miaka 17 na siku 40.
Kabla ya kuitwa kwenye kikosi cha Ireland Kaskazini kwa ajili ya Kombe la Dunia 982 na kocha Billy Bingham, Whiteside alikuwa amecheza mechi mbili tu za timu ya wakubwa ya Manchester United. Hata hivyo, tayari alikuwa ameweka rekodi ya kuwa mfungaji mdogo zaidi wa klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa 1981-82.
Katika mchezo wa kwanza wa taifa lake kwenye mashindano hayo ambayo yalikuwa mara yao ya kwanza kushiriki baada ya miaka 24 Whiteside alivunja rekodi ya Kombe la Dunia. Hakufunga bao katika mchezo huo, lakini alipata kadi ya njano na hivyo kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuonywa katika historia ya mashindano hayo.
Cha kushangaza, Ireland Kaskazini ilifika robo fainali mwaka huo ikiwemo ushindi maarufu wa bao 1-0 dhidi ya Hispania kabla ya kuondolewa na Ufaransa iliyoongozwa na Michel Platini. Whiteside alirejea tena Kombe la Dunia 1986 na kufunga bao dhidi ya Algeria katika sare ya 1-1. Hata hivyo, timu yao haikufanikiwa kusonga mbele. Kwa masikitiko, majeraha ya goti yalimlazimisha kustaafu soka akiwa na miaka 26 alipokuwa akiichezea Everton. Aliichezea Ireland Kaskazini mechi 39 na kufunga mabao tisa.
Samuel Eto’o miaka 17 na siku 98
Katika mechi kati ya Cameroon dhidi ya Italia iliyochezwa Juni 17, 1998 siku ileile ambayo Whiteside aliweka rekodi miaka 16 kabla yake, Samuel Eto’o aliingia kwenye historia kwa kuwa mmoja wa wachezaji wadogo zaidi kucheza Kombe la Dunia wakati Cameroon ilipofungwa 3-0 na Italia.
Huo haukuwa mwanzo wake katika timu ya taifa kwani alikuwa tayari ameichezea Cameroon kabla hata hajafikisha miaka 16. Mashindano hayo yalikuwa ya kwanza kati ya Kombe la Dunia manne aliyoshiriki.
Ingawa 1998 alicheza dakika 24 pekee, mwaka 2002 matumaini yalikuwa makubwa kwake baada ya kushinda mataji mawili mfululizo ya Afcon na medali ya dhahabu ya Olimpiki. Hata hivyo, Cameroon haikufika mbali licha ya Eto’o kufunga dhidi ya Saudi Arabia. Baadaye aliendelea kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Cameroon akiwa na mabao 56. Mabao mawili tu aliyafunga katika Kombe la Dunia na alistaafu soka la kimataifa 2014 akiwa amecheza mechi 118.
Femi Opabunmi miaka 17 na siku 100
Licha ya kwamba Kombe la Dunia 2002 halikuwa zuri kwa Nigeria baada ya kufungwa na Argentina pamoja na Sweden, lakini mchezo wa Nigeria dhidi ya England uliopigwa Juni 12, 2002 ndio uliokuwa wake. Hata hivyo, sare ya 0-0 dhidi ya England ilimfanya Femi Opabunmi kuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Opabunmi alikuwa ameonyesha kiwango kizuri katika Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 mwaka mmoja kabla, ikiwemo kufunga hat-trick dhidi ya Australia. Alionekana kuwa na mustakabali bora, huku klabu kama Manchester United, Arsenal na Lyon zikimtaka. Lakini ndani ya miaka minne alilazimika kustaafu kutokana na matatizo ya macho yaliyosababisha glaucoma (magonjwa ya macho yanayoharibu neva ya macho, hali ambayo mara nyingi inahusishwa na shinikizo kubwa ndani ya jicho, na ni moja ya sababu kuu zinazoweza kusababisha upofu wa kudumu) na hatimaye kupoteza uwezo wa kuona kwa jicho moja.
Salomon Olembe miaka 17 na siku 184
Olembe aling’ara katika mchezo wa Cameroon dhidi ya Austria uliochezwa Juni 11, 1998 na hii ilikuwa siku sita kabla ya Eto’o kucheza mechi yake ya kwanza Kombe la Dunia, ambapo alikuwa tayari ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi wa Cameroon kucheza mashindano hayo.
Olembe aliingia kwenye timu ya taifa akiwa na miaka 16 na akaendelea kung’ara akiwa Nantes nchini Ufaransa. Katika Afcon 1998, alitoa pasi ya bao katika mchezo wake wa kwanza. Ingawa alicheza mechi tatu tu za Kombe la Dunia katika maisha yake, aliendelea kuitumikia Cameroon kwa mechi 65 na kushinda Afcon 2000 na 2002.
Pele miaka 17 na siku 234
Mechi kati ya Brazil dhidi ya Urusi iliyopigwa Juni 15, 1958 ilimtoa Pele na ndiye aliyeshikilia rekodi ya mchezaji mdogo kwa muda mrefu na bado anashikilia rekodi nyingi za mchezaji mdogo zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.
Baada ya kupona jeraha la goti lililomuweka nje mwanzoni mwa mashindano 1958 nchini Sweden, Pele alianza kung’ara dhidi ya Urusi siku hiyo. Katika robo fainali dhidi ya Wales, alifunga bao lake la kwanza na kuwa mfungaji mdogo zaidi katika historia ya michuano hiyo. Katika ushindi wa 5-2 dhidi ya Ufaransa kwenye nusu fainali alifunga hat-trick na kuweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia.
Brazil iliifunga Sweden 5-2 fainali na Pele akafunga mabao mawili, akiwa mchezaji mdogo zaidi kucheza na kufunga katika fainali ya Kombe la Dunia akiwa na miaka 17 na siku 249. Baadaye alishiriki Kombe la Dunia mara nne na kushinda mara tatu. Pia alifunga mabao 12 katika historia ya mashindano hayo na kuweka rekodi ya pasi nyingi za mabao katika mashindano 1970.