Simba SC

KOCHA MGOSI ASEMA MAKOSA YAMEISHA SASA NI UBINGWA

Vardo May 29, 2026 10:09 am

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mussa Mgosi, amesema kikosi chake kimejifunza masomo muhimu kutokana na makosa yaliyotokea katika michezo ya hivi karibuni, na sasa kimeelekeza nguvu zote kuhakikisha kinapata ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Mashujaa Queens, hatua inayolenga kukaribia zaidi ndoto ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mgosi amesema mchezo wa hivi karibuni dhidi ya Tausi Queens ulikuwa na matarajio makubwa ya Simba kuondoka na ushindi na kutangaza dhamira yao ya ubingwa, lakini matokeo yakaacha funzo muhimu kwa benchi la ufundi pamoja na wachezaji kuhusu umuhimu wa umakini katika kila dakika ya mchezo.

Ameeleza kuwa changamoto zilizojitokeza katika mchezo huo zimekuwa darasa muhimu ambalo sasa limetumika kuboresha maandalizi kuelekea mchezo ujao dhidi ya Mashujaa Queens utakaopigwa Mei 31 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

“Tumeenda na akili ya kutangaza ubingwa, lakini sasa tunaenda kusahihisha makosa yetu. Haya yanatufundisha kuja na akili ya mechi ya kushinda, lazima tushinde,” amesema Mgosi.

Ameongeza kuwa katika hatua hizi za mwisho wa msimu, hakuna nafasi ya kupoteza umakini kwani kila mchezo una uzito mkubwa katika kuamua hatma ya ubingwa, hususan kwa timu zinazoendelea kushindana vikali kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kocha huyo amesisitiza kuwa Simba ina kikosi chenye uwezo wa kufanya vizuri hadi mwisho wa msimu, lakini mafanikio yatategemea zaidi nidhamu, matumizi sahihi ya nafasi za kufunga, na umakini katika dakika zote 90 za mchezo

“Tuweze kupata ubingwa, ubingwa wa Simba tutaupata kwa kuhakikisha tunatumia nafasi na kushinda,” ameongeza.

Kauli hiyo inaashiria dhamira mpya ndani ya Simba SC kuelekea hatua za mwisho za msimu, huku mashabiki wakisubiri kuona kama timu yao itaweza kurejea kwenye kiwango bora na kuongeza kasi katika mbio za ubingwa.

DIARRA AKITELEZA TU, KASSALI TAYARI KUMSHUSHA KILELENI