KMC FC

KIUNGO WA KMC FC MLANGONI JKT TANZANIA

Vardo June 7, 2026 8:23 pm

WAKATI KMC FC ikibakisha hatua chache kucheza Ligi ya Championship msimu ujao wa 2026-2027, nyota wa timu hiyo, Rashid Chambo ameanza kuzivutia klabu mbalimbali ili kuipata saini yake, huku maafande wa JKT Tanzania ikiwa mstari wa mbele.

Nyota huyo wa zamani wa Coastal Union na Dodoma Jiji, mkataba wake na KMC unafikia tamati rasmi Juni 30, 2026, ambapo kwa hali ya kikosi hicho kitakachoshiriki Ligi ya Championship msimu ujao, kuna uwezekano mdogo wa kuendelea kukichezea.

Katika Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026, KMC inaburuza mkiani mwa msimamo ikiwa nafasi ya 16 na pointi zake tisa tu, baada ya kushinda mechi mbili, ikitoka sare tatu na kupoteza 20 kati ya 25 iliyocheza, ikifunga mabao 13 na kuruhusu 43.

Licha ya kiwango kisichoridhisha kwa timu hiyo, ila Chambo amechangia mabao sita ya Ligi Kuu akiwa kikosini humo, baada ya kufunga matatu na kuasisti pia matatu, jambo linalomweka katika nafasi ya kuondoka pindi tu mkataba wake utakapoisha.

Akizungumza na Soka la Bongo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC (CEO), Daniel Madenyeka amesema kwa sasa ni ngumu kuzungumzia suala la wachezaji wanaomaliza mikataba yao, kutokana na nafasi mbaya iliyo timu hiyo ya kujinasua na kutoshuka daraja.

“Ni ngumu kuzungumzia hilo kwa sasa kutokana na nafasi tuliyopo, tathimini ya kina kiujumla tutaifanya baada ya msimu kumalizika, ninachowaomba mashabiki zetu waendelee kutuunga mkono licha ya mwenendo usioridhisha,” amesema Madenyeka.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua nyota huyo anayeweza kucheza mshambuliaji wa kati na wakati mwingine akitokea pembeni kwa maana ya winga ya kulia na kushoto kwa ufasaha, ni miongoni mwa wachezaji wanaopigiwa hesabu za kutua JKT Tanzania.

BILO, RUANGWA WAREJEA WALIKOTOKA GEITA GOLD, KAGERA SUGAR ZAREJEA LIGI KUU BARA