Azam FC Yafunguka Mkataba wa Fei Toto: “Tupo Tayari Kufanya Biashara”
Uongozi wa klabu ya Azam FC umevunja ukimya na kuweka wazi msimamo wake kuhusu hatma ya kiungo mchezeshaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kufuatia kuendelea kusambaa kwa tetesi zinazomhusisha na kuondoka klabuni hapo.
Azam FC imesisitiza kuwa haijapokea taarifa yoyote rasmi kutoka kwa mchezaji huyo au klabu nyingine inayomtaka, ikibainisha kuwa Fei Toto bado ana mkataba wa muda mrefu na anaendelea na maandalizi ya msimu mpya wa 2026/27.
“Hatuna Tatizo na Mchezaji Anayeondoka” – Hashimu Ibwe
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa Azam FC, Hashimu Ibwe, ameeleza kuwa klabu hiyo haijamfunga mikono mchezaji yeyote, lakini taratibu halali za usajili lazima zifuatwe.
“Hatuna tatizo na mchezaji anayetaka kuingia au kuondoka. Klabu haina taarifa yoyote kuhusu Fei Toto kuondoka. Ni mchezaji wa Azam FC mwenye mkataba wa muda mrefu. Kama kuna timu inamhitaji, milango ipo wazi ije kufanya biashara nasi. Hatumzuii mchezaji kuondoka endapo taratibu zitafuatwa,” amesema Ibwe.
Nyota Wote Wapo Kambini, Safari ya Rwanda Julai 30
Ibwe ameongeza kuwa wachezaji wote wanaotajwa kwenye tetesi za usajili tayari wameripoti kambini na wanaendelea na programu za benchi la ufundi, jambo linalothibitisha kuwa bado ni sehemu ya mipango ya timu hiyo.
Kikosi cha Azam FC kinatarajiwa kuondoka nchini Julai 30 kuelekea Rwanda kwa ajili ya kambi maalumu ya maandalizi ya pre-season kabla ya kuanza kwa mashindano rasmi ya msimu wa 2026/27.