BILO, RUANGWA WAREJEA WALIKOTOKA
WAKATI bingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake, Simba Queens akitangazwa mapema huku kwenye vita ya kushuka daraja nako ishajulikana nani ana nafasi ya kusalia na nani anarudi Ligi daraja la kwanza.
Kwa msimamo wa ligi baada ya raundi ya 20, Bilo FC ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 11, huku Ruangwa Queens ikishika mkiani ikiwa na pointi tisa.
Hata kama timu hizo zitashinda mechi zote mbili zilizobaki, zitafikia pointi 17 na 15 mtawalia, idadi ambayo haiwezi kuzifikia timu zilizo mbele yao ambazo tayari zimejikusanyia pointi nyingi zaidi.
Hiyo ina maana kuwa Bilo FC na Ruangwa Queens tayari zimepoteza vita ya kubaki Ligi Kuu na sasa zinajiandaa kurejea Ligi Daraja la Kwanza, ambako ndiko zilipotokea kabla ya kupanda msimu huu.
Msimu huu ulishuhudiwa timu 12 zilizokuwa zinashindania taji la malkia, timu nne kutoka Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Geita Queens, Tausi FC, Bilo FC na Ruangwa Queens zilizochuana kwenye michuano hiyo zilipanda moja kwa moja.
Hata hivyo, wakati Geita Queens na Tausi FC zikionyesha uwezo wa kuhimili ushindani na kujitengenezea nafasi ya kubaki kwenye ligi, Bilo FC na Ruangwa Queens zimeshindwa kuendana na kasi ya mashindano na sasa zinarejea zilipotoka baada ya kudumu msimu mmoja.
Bilo kwenye mechi 20 imeshinda mechi tatu sare mbili na kupoteza mechi 15, Ruangwa ambayo imecheza mechi 19 imeshinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi 14.