Habari za michezo

Mexico Yatangulia 16 Bora, Ikiisubiri England u DR Congo

Vardo July 1, 2026 10:38 am

MEXICO CITY, MEXICO: WENYEJI wenza wa michuano ya Kombe la Dunia, Mexico imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kuichapa Ecuador mabao 2-0, katika mechi kali na ya kuvutia ya hatua ya 32 bora.

Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azteca, jijini, ilichelewa kuanza kwa zaidi ya saa moja tofauti na muda uliopangwa kutokana na dhoruba kali ya radi na ngurumo iliyotanda uwanjani hapo.

Hata hivyo, hali hiyo ya hewa haikuwa shida kwa wenyeji kwani Iliwachukua dakika 22, kutangulia kufunga bao kali la kwanza lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Julian Quinones aliyemalizia pasi ya Roberto Alvarado.

Wakati Ecuador ikitafakari namna bora ya kusawazisha, mshambuliaji Raul Jimenez akaifungia Mexico bao la pili dakika ya 31, baada ya muunganiko mzuri wa kiuchezaji kati yake na nyota mwenzake kikosini, Julian Quinones.

Bao la Jimenez ni la 47 kuifungia timu hiyo, akishika nafasi ya pili kwa nyota waliofunga mabao mengi ya kikosi cha Mexico, nyuma ya Javier Hernandez ‘Chicharito’  anayeongoza akiwa na 52.

Mabao hayo mawili yalitokana na timu hiyo kutumia vyema nafasi za kufunga vizuri kwani ndio mashuti yaliyolenga lango la wapinzani wao na kuwapeleka mapumziko wakiongoza, huku wakicheza pia soka nzuri.

Kipindi cha pili Ecuador ikaanza kwa kasi ya umiliki wa mpira, ikijaribu kupambana kusawazisha mabao hayo, lakini uimara wa safu ya beki ya Mexico iliwanyima nafasi na mwishowe ikaaga michuano.

Matumaini ya kusawazisha mabao hayo yalionekana magumu zaidi kwa Ecuador, baada ya beki wa timu hiyo, Piero Hincapie kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 90+5 na jahazi hilo kuzidi kudidimia.

Matokeo hayo yanaifanya Mexico iwe ni timu ya pili kati ya tatu zinazoandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026 kufuzu hatua ya 16 bora, baada ya Canada iliyotangulia awali baada ya kuifunga Afrika ya Kusini bao 1-0, Juni 28.

Ushindi huu kwa Mexico unaifanya kusubiri mshindi wa mechi ya leo saa 1:00 usiku kati ya England dhidi ya DR Congo ili kujua mpinzani wake atakayecheza naye katika hatua ya 16 bora.

Mexico ilianza kushiriki fainali za Kombe la Dunia mara ya kwanza mwaka 1930, zilizofanyika Uruguay na wenyeji kutwaa ubingwa. Mwaka huu inaanda kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mwaka 1970, 1986 na 2026.

Katika miaka yote iliyoandaa,  ilifika hadi hatua ya robo fainali, ikianza mwaka 1970 na 1986, huku mafanikio mengine ni kuishia 16, bora mara saba kuanzia 1994, 1998, 2002, 2006, 2010, 2014 na 2018.

Kwa upande wa Ecuador imekuwa ni timu inayoimarika taratibu kutoka Bara la Amerika Kusini na inashiriki fainali hizi ikiwa ni mara ya tano tangu mwaka 2002, 2006, 2014, 2022 na 2026.

Mafanikio bora ya timu hiyo ni katika fainali za mwaka 2006, zilizofanyika Ujerumani na  ilifika hatua ya 16 bora na kutolewa na England kwa kuchapwa bao 1-0, la Frii-Kiki ya David Beckham dakika ya 60.

Fainali nyingine ilizoshiriki,  mwaka 2002, 2014 na 2022 iliishia makundi kisha mwaka huu wa 2026, kufika hadi hatua ya 32 bora.

Steve Barker: Msimu Ujao ni Wakati wa Kuvuna Mataji Simba SC JKT Tanzania Yaomba Radhi, Yampa Pole Pacome