Simba Yaelekeza Macho Kombe La Shirikisho, Waamuzi Gumzo
MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema benchi la ufundi na wachezaji wa klabu hiyo walitimiza wajibu wao kwa kiwango cha juu katika msimu wa 2025/26, licha ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akidai baadhi ya maamuzi ya waamuzi yaliinyima timu hiyo nafasi ya kutwaa taji.
Ahmed amesema Simba ilipoteza pointi muhimu katika baadhi ya mechi ambazo, kwa mtazamo wa klabu hiyo, haikustahili kupoteza. Alidai maamuzi yaliyotolewa na waamuzi katika baadhi ya michezo yalikuwa na athari kubwa katika mbio za ubingwa.
Ameongeza kuwa kulikuwa na maamuzi ambayo hayakuwa ya haki, huku mengine akidai yalifanywa kwa makusudi, jambo ambalo lilichangia kuathiri safari ya Simba kuelekea kileleni mwa msimamo.
“Sisi kwetu, benchi la ufundi na wachezaji wametimiza majukumu yao ipasavyo kwa asilimia 100. Yote yaliyotokea kuna watu walikuwa wamekaa pembeni na kufanya makusudi,” amesema Ahmed.
Ingawa hakuwataja moja kwa moja watu aliokuwa akiwalenga, Ahmed amesisitiza kuwa Simba imejikuta ikikumbana na mazingira ambayo hayakuwa ya ushindani wa haki katika baadhi ya mechi za msimu uliomalizika.
Pamoja na hayo, amesema uongozi wa klabu umeanza kufanya tathmini ya kina ya msimu mzima ili kubaini maeneo yaliyohitaji maboresho, akieleza kuwa lengo ni kuijenga Simba yenye ushindani mkubwa zaidi kuelekea msimu wa 2026/27.
Ahmed pia amefafanua kuwa kwa upande wa Simba, msimu bado haujahitimishwa rasmi kwani macho na nguvu zote sasa zimeelekezwa kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Azam FC, wakilenga kumaliza kampeni za msimu kwa kutwaa taji hilo.
Amesisitiza kuwa baada ya mashindano yote kukamilika, Simba itaanza maandalizi ya kina kwa ajili ya msimu ujao, ikiwa na azma ya kurejea kwa nguvu, kupigania mataji ya ndani na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa.