Simba Haijakata Tamaa, CEO Aahidi Makubwa 2026/2027
UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/26, hakutayumbisha mipango ya klabu hiyo, badala yake changamoto walizopitia zitakuwa msingi wa kuijenga timu imara zaidi kuelekea msimu ujao.
Simba ilihitimisha msimu ikiwa nafasi ya pili na alama 73, tofauti ya alama mbili pekee nyuma ya mabingwa Yanga, baada ya mbio za ubingwa zilizoamuliwa katika mechi ya mwisho wa msimu.
Akizungumza baada ya msimu wa Ligi kutamatika, Mkurugenzi Mtendaji wa Simba, Zubeda Sakuru, amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki kwa moyo wa kujitolea na mapambano waliyoonyesha, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kukata tamaa licha ya kukosa ubingwa.
“Hakuna sababu ya kuinamisha vichwa. Kila mmoja ndani ya Simba alitimiza wajibu wake kwa kujituma tangu mwanzo hadi mwisho wa msimu. Wachezaji na benchi la ufundi waliheshimu nembo ya klabu kwa kupambana katika kila mechi,” amesema Zubeda.
Ameongeza kuwa mafanikio ya kweli hujengwa kwa mshikamano, uvumilivu na kujifunza kutokana na changamoto, akisisitiza kuwa yaliyotokea msimu huu yataifanya Simba irejee ikiwa na nguvu na ushindani mkubwa zaidi.
“Changamoto tulizokutana nazo zitakuwa chachu ya kuijenga Simba yenye nguvu zaidi katika misimu ijayo. Tutarejea tukiwa bora zaidi na tayari kupigania mafanikio makubwa,” amesisitiza.
Zubeda pia ameatuma salamu za faraja mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi, akiwataka waendelee kuwa na imani na timu yao huku akiahidi kuwa safari ya kurejea kileleni tayari imeanza.
“Kwetu nyinyi ni mabingwa wa heshima. Ni suala la muda tu, Simba ya kweli ya wananchi itarejea kileleni,” amesema.
Kauli hiyo imeamsha matumaini mapya kwa mashabiki wa Simba, huku macho sasa yakielekezwa kwenye maandalizi ya msimu wa 2026/27, ambao klabu hiyo inalenga kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa.