MIlioni 750, Zatua kwa Oura, Barker Ang’ang’ania Abaki Simba
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Anicet Oura, ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji wanaowindwa na vilabu vya Ulaya baada ya kuvutia timu tatu ambazo ni Bursaspor ya Uturuki, Víkingur Reykjavík ya Iceland na DAC 1904 Dunajská Streda ya Slovakia.
Nyota huyo raia wa Ivory Coast alijiunga na Simba Januari mwaka huu akitokea IF Gnistan ya Finland kwa mkataba wa miaka miwili.
Tangu alipotua Msimbazi, amekuwa akionyesha kiwango cha juu kilichomfanya kuwa tegemeo muhimu katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Katika msimu wake wa kwanza akiwa Simba, Oura alitoa mchango mkubwa kwa kuisaidia timu kutwaa Kombe la CRDB na Kombe la Muungano.
Aidha, alifunga mabao sita na kutoa pasi tatu za mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akiisaidia Simba kumaliza msimu katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 73, tofauti ya pointi mbili nyuma ya mabingwa Yanga.
Kiwango chake pamoja na uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali za ushambuliaji kimeendelea kuongeza thamani yake sokoni, hali iliyozifanya klabu hizo za Ulaya kuonyesha nia ya kuipata saini yake kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Taarifa zinaeleza kuwa Bursaspor ndiyo inayoongoza katika mbio za kumsajili Oura, ikiwa tayari kuwasilisha ofa ya euro 250,000, sawa na zaidi ya Sh milioni 750, kwa lengo la kumshawishi Simba kumuuza.
Wakala wa mchezaji huyo, Serkan Dag, amethibitisha kuwepo kwa ofa hizo, akisema mazungumzo yanaendelea na uamuzi wa mwisho utafikiwa kwa ushirikiano kati ya mchezaji na uongozi wa Simba.
Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, anaripotiwa kutokuwa tayari kumpoteza Oura kwa sasa, akimtaja kuwa sehemu muhimu ya mipango yake kuelekea msimu wa 2026/27 kutokana na ubora wake, nidhamu na mchango mkubwa anaoutoa ndani ya kikosi.
Pamoja na kuvutiwa na vilabu vya Ulaya, hatma ya Oura bado haijafahamika, huku uongozi wa Simba ukiendelea kukaa kimya kuhusu mustakabali wa kiungo huyo ambaye bado amebakiza takribani mwaka mmoja na nusu kwenye mkataba wake.