news

Chuga Boy Aipa Kisogo KAA Gent, Kisa Mamillion Ya Yanga

Vardo July 14, 2026 7:01 pm

KITENDO cha Yanga kuweka mezani dau nono kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Fountain Gate FC, Juma Abushiri ‘Chuga Boy’, kimeonekana kubadili mwelekeo wa safari yake ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya KAA Gent ya Ubelgiji.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamepiga hatua kubwa katika harakati za kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu wa 2026/27, huku taarifa zikieleza kuwa tayari wamefikia makubaliano ya awali na nyota huyo.

Inaelezwa kuwa Chuga Boy tayari amewasili Dar es Salaam, ambapo Yanga inamtafutia makazi ya muda akisubiri kukamilisha taratibu za mwisho na kutambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kiungo huyo amekubali kusaini mkataba wa miaka mitatu utakaomuweka Yanga hadi mwaka 2029. Chini ya makubaliano hayo, anatarajiwa kulipwa mshahara wa Sh5 milioni kwa mwezi pamoja na ada ya usajili (sign-on fee) inayodaiwa kufikia Sh90 milioni.

Chanzo cha karibu na mazungumzo hayo kimeeleza kuwa Yanga ilifanya kazi kubwa kuhakikisha inampata mchezaji huyo, ikiwemo kufanya mazungumzo na familia yake ili kupata ridhaa ya kukamilisha uhamisho huo.

Taarifa zinaongeza kuwa mama wa Chuga Boy ameridhia uamuzi wa mwanawe kujiunga na Yanga, jambo lililosaidia kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikichelewesha kufungwa kwa dili hilo.

Wakati huohuo, Fountain Gate FC bado ina nafasi ya kumpeleka mchezaji huyo KAA Gent ya Ubelgiji kwa ajili ya majaribio ikiwa itaamua kuendeleza mchakato huo.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Chuga Boy ameonyesha nia ya kuendelea na soka lake ndani ya Yanga, hali inayowapa mabingwa hao matumaini makubwa ya kukamilisha usajili huo katika muda mfupi ujao.

Yanga inaendelea na mpango wa kuimarisha kikosi chake kwa lengo la kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa msimu wa 2026/27.

Messi Amwakia Mwamuzi Pinheiro Yanga Yapata Nafuu, FIFA Yaiondolea Adhabu Ya Usajili