Jumatatu Ni Mwanzo Wa Safari Mpya Yanga Chini Ya Mngqithi
KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Jumatatu, Julai 20, 2026, kuanza rasmi maandalizi ya msimu wa 2026/27, huku kocha mkuu mpya, Manqoba Mngqithi, akitarajiwa kuanza kazi yake rasmi baada ya kutambulishwa na mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, wachezaji wote wanatakiwa kuripoti kambini siku hiyo mapema kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya, hatua ambayo itafungua rasmi maandalizi ya msimu mpya.
Kamwe amesema baada ya kukamilisha vipimo hivyo, kikosi kitaingia kambini moja kwa moja na kuanza programu ya mazoezi chini ya Mngqithi, ambaye amepewa jukumu la kuiongoza Yanga katika mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.
“Timu itaripoti Julai 20 na kambi itakuwa Avic Town. Wachezaji wote watawasili siku hiyo na watafanyiwa vipimo vya afya kabla ya kuingia kambini rasmi,” amesema Kamwe.
Ameeleza kuwa Yanga inaingia msimu mpya ikiwa na malengo makubwa ya kuendeleza mafanikio yake, baada ya kufanya maboresho ya kikosi kupitia usajili wa wachezaji wenye ubora na uzoefu wa kuongeza ushindani katika nafasi mbalimbali.
Kamwe amesema uongozi una imani kikosi kilichoundwa kitakuwa na ushindani mkubwa zaidi kuliko misimu iliyopita, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona Yanga ikianza safari ya msimu wa 2026/27 kwa nguvu mpya chini ya benchi jipya la ufundi la Mngqithi.