Yanga SC

Mngqithi Awasili Na Timu Yake, Moalin Yupo Sana

Vardo July 15, 2026 10:04 am

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi muundo wa benchi la ufundi kuelekea msimu wa 2026/27, ukithibitisha kuwa kocha wa muda, Abdihamid Moalin, ataendelea kuwa sehemu ya kikosi hicho kama kocha msaidizi wa pili chini ya kocha mkuu mpya, Manqoba Mngqithi.

Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Msemaji wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, alisema ujio wa Mngqithi unaambatana na baadhi ya wataalamu wake, lakini Moalin ataendelea kubaki ndani ya benchi la ufundi ili kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa kazi iliyokuwa ikifanywa.

Kamwe amesema Yanga inalenga kuwa na benchi la ufundi lenye wataalamu wengi na wenye majukumu tofauti, mfano wa vilabu vikubwa vya Afrika na Ulaya, hatua ambayo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa kuifanya timu iwe na ushindani mkubwa msimu ujao.

Ameeleza kuwa Mngqithi anatarajiwa kuwasili na kocha msaidizi wa kwanza pamoja na mchambuzi mmoja wa video, huku Yanga ikiendelea kubaki na mchambuzi mwingine aliyekuwa ndani ya benchi la zamani ili kuimarisha uchambuzi wa mechi na kudumisha mwendelezo wa utendaji.

“Baada ya kuja kocha mpya, kuna makocha wengine wanakuja naye. Moalin ataendelea kubaki kama kocha msaidizi wa pili. Kocha mkuu anakuja na kocha msaidizi namba moja pamoja na video analyst mmoja, huku mwingine akiendelea kutoka kwenye benchi la zamani,” amesema Kamwe.

Kuhusu kocha wa viungo, Tshephang “Chyna” Mokaila, Kamwe amesema klabu bado ipo kwenye mazungumzo naye baada ya mkataba wake kumalizika.

Amebainisha kuwa Mngqithi anamfahamu vizuri na ameomba juhudi zifanyike ili aendelee kubaki, lakini endapo mazungumzo hayatakuwa na mafanikio, kocha mkuu atapendekeza mbadala wake.

Meridianbet Yabisha Hodi Hospitali Ya Wilaya Kinondoni, Mabwepande Jumatatu Ni Mwanzo Wa Safari Mpya Yanga Chini Ya Mngqithi