Simba SC

Simba Yashinda Vita Ya Mwalimu, Azam Yaambulia Patupu

Vardo July 15, 2026 10:11 am

SIMBA imefanikiwa kushinda vita ya kumbakiza mshambuliaji Mtanzania, Selemani Mwalimu, baada ya kufikia makubaliano na Wydad Athletic ya Morocco ya kuendelea kumiliki huduma zake kwa mkopo wa msimu mmoja zaidi wa 2026/27.

Hatua hiyo imezima ndoto za Azam FC, ambao pia walikuwa wakihitaji saini ya mshambuliaji huyo. Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa kati ya Simba na Wydad yameihakikishia klabu hiyo kuendelea kuwa na nyota huyo aliyekuwa na mchango mkubwa msimu uliopita.

Tangu atue Msimbazi, Mwalimu ameonyesha kiwango bora na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha kocha Steve Barker. Uwezo wake wa kufunga mabao na kucheza kwa kujituma ulimfanya kuwa tegemeo katika mashindano mbalimbali ya ndani.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa Wydad imekubali ombi la kuongeza muda wa mkopo wa mshambuliaji huyo, jambo litakalompa Barker nafasi ya kuendelea kumjumuisha katika mipango yake ya kuijenga timu kuelekea msimu mpya.

“Mwalimu ameonyesha kiwango cha kuvutia tangu ajiunge na Simba. Amefunga mabao 15 katika mashindano mbalimbali na amekuwa miongoni mwa wachezaji waliobeba matumaini ya mashabiki kutokana na mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji,” alisema chanzo hicho.

Kuendelea kubaki kwa Mwalimu ni sehemu ya mkakati wa Simba wa kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la CAF na mashindano mengine ya kimataifa. Uongozi unaamini uimara wa kikosi hicho utaiwezesha timu kuwa na ushindani mkubwa na kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita.

Jumatatu Ni Mwanzo Wa Safari Mpya Yanga Chini Ya Mngqithi O’reilly:  Nafurahi Kumkabili Messi