Kevin Keegan afariki dunia
Habari za michezo

Gwiji wa Liverpool na Newcastle Kevin Keegan Afariki Dunia Akiwa na Miaka 75

Vardo July 20, 2026 7:03 pm

Ulimwengu wa soka umezama kwenye simanzi kufuatia kifo cha mchezaji na kocha wa zamani wa Liverpool, Hamburg, Southampton na Newcastle United, Kevin Keegan, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 baada ya kuugua saratani ya tumbo.

Familia ya Keegan imethibitisha taarifa hizo, ikieleza kuwa gwiji huyo alifariki dunia akiwa amezungukwa na watu wake wa karibu.

Keegan aligundulika kuwa na saratani ya tumbo ya hatua ya nne (Stage 4) mwezi Januari mwaka huu, baada ya kulazwa hospitalini kutokana na maumivu makali ya tumbo yaliyomsumbua kwa muda mrefu. Licha ya changamoto za kiafya, mara ya mwisho alionekana hadharani Mei 31 akiwa mwenye tabasamu na uchangamfu.

Rafiki yake wa karibu, Peter Graves, alitangaza kifo hicho kwa huzuni kubwa akisema:

“Kwa masikitiko makubwa tunatangaza kuwa Kevin Keegan amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.”


Hamu Yake ya Mwisho Kuaga Newcastle

Mwezi Mei, akiwa katika Ukumbi wa Tyne Theatre, Keegan alieleza nia yake ya kutaka kupata nafasi ya kuaga rasmi mashabiki wa Newcastle United kwenye Uwanja wa St James’ Park.

Akizungumza na Graves, Keegan alisema:

“Nataka kusema kwaheri. Sikupata nafasi hiyo nilipoondoka Newcastle mara ya mwisho.”

Kauli hiyo sasa imebaki kuwa moja ya maneno yake ya mwisho yaliyogusa hisia za wengi kabla ya mauti kumfika.


Utani Kuhusu Ugonjwa Wake na Mapenzi kwa Liverpool

Keegan, ambaye alishinda tuzo ya mchezaji bora duniani (Ballon d’Or) mara mbili mfululizo (1978 na 1979), aliwahi kusimulia mazungumzo yake na daktari aliyekuwa akimtibu.

“Waliniambia wana daktari bingwa mwenye mbinu mpya za kupambana na saratani ya hatua ya nne,” alisema Keegan. Kwa utani uliogusa mioyo ya wengi, aliongeza:

“Daktari huyo alikuwa shabiki wa Liverpool, hivyo nilikwenda kukutana naye. Nilijua sitatembea peke yangu (You’ll Never Walk Alone).”


Mchango na Historia Yake Kwenye Soka

Keegan anasalia kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea nchini England. Mafanikio yake ya kushinda Ballon d’Or mara mbili mfululizo yanatambulika kama miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi kwa mchezaji kutoka Uingereza.

Baada ya kutundika daluga, aliandika historia nyingine kama kocha wa Newcastle United miaka ya 1990, ambapo aliifanya timu hiyo kucheza soka la kuvutia na kushindania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League).

Kifo cha Kevin Keegan kimeacha pengo kubwa katika ulimwengu wa mchezo wa mpira wa miguu, lakini mchango wake utaendelea kukumbukwa daima.

Nathan Chilambo Atua Simba SC Kuimarisha Beki Ya Kulia Mlandege FC Yafanya Mabadiliko Makubwa: Yatemema Nyota 18 Msimu wa 2026/27