KVZ Kagame Cup
Michezo Bongo

KVZ Kagame Cup: Ujumbe Mzito Wa Waziri Pembe Kwa Mabingwa Wa Zanzibar

Vardo July 20, 2026 7:22 pm

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Juma Pembe, amewataka wachezaji wa timu ya KVZ FC kupambana kufa na kupona ili kulinda na kuheshimisha jina la Zanzibar katika mashindano ya Kagame Cup 2026 nchini Rwanda.

Waziri Pembe aliyasema hayo Julai 19, 2026, wakati akiaga rasmi kikosi hicho kinachojiandaa kuanza kipakipiki cha mashindano hayo yanayotazamiwa kutimua vumbi kuanzia Julai 24, 2026.

“Mnaenda Kushindana, Sio Fanya Majaribio”

Akiwapa hamasa wachezaji hao, Pembe alikazia kuwa Zanzibar ipo mabegani mwao na wanapaswa kucheza kwa kujiamini bila uoga wowote.

“Nawataka mcheze mpira bila uoga. Huko hamuendi kufanya majaribio, badala yake mnaenda kushindana. Hivyo nahitaji muwe tayari kuipigania nchi,” alisisitiza Waziri Pembe.

Mbali na hayo, aliuasa msafara huo kudumisha na kulinda maadili pamoja na tamaduni za Zanzibar wakiwa nchini Rwanda.

Kundi Vigumu, Lengo Ni Ligi Ya Mabingwa Afrika

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Mkuu wa Kikosi cha KVZ, Kanali Said Ali Shamhuna, alikiri kuwa wamo kwenye kundi gumu lenye mabingwa wa nchi mbalimbali, lakini akaahidi kuwa KVZ itatoa burudani na ushindani wa tofauti.

Kanali Shamhuna alibainisha kuwa, baada ya uwekezaji wa zaidi ya miaka 22, hatimaye timu hiyo imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (2025/2026) na sasa ipo tayari kuandika historia mpya kimataifa. Msafara wa KVZ kuelekea Rwanda una jumla ya watu 48, wakiwemo wachezaji na viongozi. Kwa mashabiki waliopo nyumbani, michezo yote itaonyeshwa kwenye runinga kubwa zitakazowekwa makao makuu ya kikosi hicho.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu Hababuu Ali alieleza kuwa mashindano haya ya Kagame Cup ni fursa adimu na kipimo tosha kuelekea maandalizi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).

Mlandege FC Yafanya Mabadiliko Makubwa: Yatemema Nyota 18 Msimu wa 2026/27 Meridianbet Sasa Ndani Ya Octagon Ya UFC