MO Dewji Na Magori Wakutana Simba SC: Mipango Ya Usajili 2026/27
DAR ES SALAAM — Rais wa Simba SC, Mohammed Dewji ‘MO’, amefanya kikao kizito cha kimkakati na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Crescentius Magori, kilicholenga kupanga safu ya ushindi kuelekea msimu wa 2026/27.
Katika kikao hicho maalumu, Magori alimpa MO Dewji taarifa ya kina juu ya hatua mbalimbali zinazoendelea ndani ya klabu, ikiwemo mchakato wa usajili wa nyota wapya wa kimataifa na wa ndani wanaotarajiwa kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho. Usajili huo unalenga kujenga timu tishio itakayotawala mashindano ya ndani (NBC Premier League) na yale ya kimataifa (CAF).
Baada ya kupokea ripoti hiyo, MO Dewji alipongeza hatua zilizofikiwa na kusisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza na kushirikiana kwa karibu na bodi pamoja na uongozi mzima wa Simba SC.
“Dhamira yetu ni kuona Simba inakuwa na kikosi imara chenye uwezo wa kushindana na kutwaa mataji yote msimu ujao,” alibainisha MO Dewji huku akimhakikishia Magori kuwa atatoa ushirikiano na rasilimali zote zinazohitajika ili kufanikisha mipango hiyo.