Simba SC Yaanza Kambi Msimu Mpya: Matola Afunguka Hali Ya Wachezaji Na Usajili Mpya
Kikosi cha Simba SC kimeanza rasmi mazoezi na maandalizi ya msimu mpya wa 2026/27 baada ya wachezaji kurejea kambini kutoka mapumziko mafupi yaliyofuata fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Azam FC.
Benchi la ufundi la Simba limeeleza kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya utimamu wa mwili wa wachezaji wote walioripoti kambini.
Akizungumzia maandalizi hayo, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema ratiba ngumu ya mwishoni mwa msimu uliopita iliwalazimu kutoa programu maalumu za mazoezi ya kibinafsi kwa wachezaji wakiwa nyumbani ili kuzuia viwango vyao kushuka.
“Baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Azam FC, mapumziko yalikuwa mafupi sana. Nawapongeza wachezaji kwa sababu kabla ya kwenda mapumzikoni tuliwapa programu za kufanya wakiwa nyumbani, na kweli wamerudi wakiwa katika hali nzuri,” alisema Matola.
Matola aliongeza kuwa nidhamu hiyo ya wachezaji imerahisisha kazi ya benchi la ufundi, kwani sasa wameanza moja kwa moja programu za kiufundi na mbinu badala ya kutumia muda mwingi kurudisha utimamu wa mwili (fitness level).
Nyota Wapya Wafiti Haraka Mfumoni
Kuhusu ingizo jipya la wachezaji waliosajiliwa hivi karibuni, Matola alibainisha kuwa nyota hao wameonyesha utayari wa hali ya juu na wameingia kwenye mfumo wa timu bila matatizo yoyote.
“Wachezaji wageni hawajaonekana kuwa wageni. Baada ya kuwaangalia na kujiridhisha kuwa wapo vizuri kimwili, sasa tunaendelea na programu nyingine za kiufundi kama tulivyopanga,” alisisitiza Matola.
Simba inaendelea na maandalizi hayo kwa kasi ya juu ikilenga kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na kimataifa kwa msimu wa 2026/27.