Yanga Yamaliza Usajili 2026/27: Yaahidi Utambulisho Wa ‘Ghafla Bin Vuu’
Yanga Yamaliza Usajili Msimu wa 2026/27, Yaahidi Utambulisho wa Kushtukiza ‘Ghafla Bin Vuu’
Uongozi wa Klabu ya Yanga umeweka wazi kuwa umekamilisha rasmi zoezi la usajili kuelekea msimu mpya wa ligi wa 2026/27, huku ukiwataka mashabiki kukaa tayari kwa utambulisho wa aina yake.
Msemaji wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, ameeleza kuwa kwa sasa nguvu zote za uongozi zimeelekezwa kwenye maandalizi ya msimu mpya baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wote waliokuwa kwenye mpango wa klabu.
Kamwe amesisitiza kuwa msimu huu hawatafuata mfumo wa kawaida wa kutambulisha wachezaji, bali watatumia mtindo wa kushtukiza utakaowapa mashabiki mshangao mkubwa.
“Tumeshamaliza zoezi la usajili. Kilichobaki sasa ni kutangaza wanaondoka na wale wanaokuja. Safari hii utambulisho wa wachezaji wetu utakuwa ‘ghafla bin vuu’. Tayari tumemtambulisha Chuga Boy (Juma Abushiri), lakini bado kuna wengine wanakuja,” alisema Kamwe.
Ameongeza kuwa lengo kuu la Yanga si kuonyesha mbwembwe za usajili, bali ni kujenga kikosi imara na chenye ushindani kitakachofanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Wakati huo huo, benchi jipya la ufundi tayari limewasili nchini na kuanza kazi mara moja. Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini leo kuanza maandalizi ya msimu mpya pamoja na kuelekea kwenye tamasha kubwa la Kilele cha Mwananchi.