Barbra Banda WAFCON 2026
Habari za michezo

Barbra Banda Aweka Rekodi Mpya WAFCON 2026: Afunga Mabao 4 Zambia Ikiiadhibu Misri 6-0

Vardo July 29, 2026 9:53 am

Nahodha na nyota wa timu ya taifa ya wanawake ya Zambia, Barbra Banda, anaendelea kuonyesha ukubwa wake katika soka la wanawake barani Afrika baada ya kuiongoza timu yake kupata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Misri katika mchezo wa Kundi C wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026), uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade Olympique de Rabat.

Banda alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Misri baada ya kupachika mabao manne peke yake. Nondo hiyo ilianza mnamo dakika ya 61 kupitia mkwaju wa penati kabla ya kuongeza bao la pili dakika tatu baadaye. Hakuishia hapo, kwani alikamilisha idadi hiyo kwa kufunga mabao mengine katika dakika ya 87 na 90.

Mabao mengine ya Zambia yaliwekwa kimiani na Racheal Nachula katika dakika ya 25 na Eneless Phiri mnamo dakika ya 90, na hivyo kuifanya Zambia kuanza vizuri mbio zao za kusaka ubingwa wa mashindano hayo.

Uwezo huo mkubwa wa Banda unazidi kuimarisha rekodi zake kwenye mashindano makubwa ya kimataifa. Hii si mara ya kwanza kwa mshambuliaji huyo kuandika historia; ikumbukwe kwenye Michezo ya Olimpiki mwaka 2021, alichapa hat-trick mbili mfululizo na kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kufanya hivyo kwenye historia ya Olimpiki.

Kwa kufunga mabao manne kwenye mechi moja ya WAFCON, Banda anajiunga na orodha ya nyota wachache waliowahi kufikia mafanikio hayo, akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Nigeria, Perpetua Nkwocha (dhidi ya Cameroon mwaka 2004) na Asisat Oshoala (dhidi ya Mali mwaka 2016).

Barker Athibitisha Ujio wa Neo Maema Simba SC Msimu Mpya Pamba Jiji Yamnyanya Beki wa JKT Tanzania, Abdulrahim Bausi Msimu Mpya