Abdulrahim Seif Bausi Pamba Jiji
Michezo Bongo

Pamba Jiji Yamnyanya Beki wa JKT Tanzania, Abdulrahim Bausi Msimu Mpya

Vardo July 29, 2026 10:04 am

Klabu ya Pamba Jiji imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi ili kurejesha ushindani wa hali ya juu, baada ya kufanikisha usajili wa beki Abdulrahim Seif Bausi aliyekuwa akikipiga JKT Tanzania msimu uliopita.

Bausi, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), Seif Bausi, amekulia kwenye mazingira ya soka na kipaji chake kilivutia hata klabu ya Simba SC msimu uliopita kabla ya JKT Tanzania kuwawahi na kumsajili.

Chanzo cha ndani kutoka Pamba Jiji kimeeleza kuwa benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Francis Baraza lilikuwa likimfuatilia kwa karibu beki huyo na kuvutiwa na uwezo wake, hivyo kuamua kumjumuisha kwenye mipango yao ya msimu ujao.

“Pamba lazima tukiimarishe kikosi. Msimu unaoanza Agosti 14 utakuwa mgumu sana kwani timu zinasajili wachezaji wa maana na ratiba ya mechi itakuwa ya karibu karibu. Ukiachana na Bausi, kuna wachezaji wengi wapya wamejiunga na timu na wengine wameondoka,” kilieleza chanzo hicho.

Mbali na soka, Bausi anamiliki Stashahada (Diploma) ya Udhibiti na Uendeshaji wa Bandari (Shipping and Port Management) kutoka Chuo cha TPA Zanzibar. Alipotafutwa kuzungumzia usajili huo, alisema kuwa masuala ya usajili ni vyema yakaachwa kwa klabu ya Pamba Jiji wenyewe kuyazungumzia.

Kwa upande wake, Kocha Francis Baraza hakutaka kuingia kwenye undani wa usajili huo na kusema: “Pamba tutatambulisha wachezaji, ila kwa sasa siwezi kumtaja mmoja mmoja. Muda utakapofika mtawajua wote kama mlivyowaona baadhi yao kwenye mitandao ya kijamii ya timu.”

Hivi karibuni, Pamba Jiji ilimtangaza kiungo mkabaji raia wa Kenya, John Ochieng ‘Champe’, aliyetokea klabu ya Zanaco FC ya nchini Zambia.

Barbra Banda Aweka Rekodi Mpya WAFCON 2026: Afunga Mabao 4 Zambia Ikiiadhibu Misri 6-0 Usajili wa Simba SC Bado Haujafungwa: Ahmed Ally Afunguka