Bodi ya Simba SC
Simba SC

Bodi ya Simba SC Yatengua Maamuzi ya Bunju: Kikao Kizito Kutajwa Kesho

Vardo August 2, 2026 11:18 pm

DAR ES SALAAM, Tanzania — Klabu ya Simba imetangaza rasmi kuwa kesho Jumatatu, Agosti 3, 2026, kutakuwa na kikao muhimu cha Bodi ya Wakurugenzi kilicholenga kujadili ajenda na tarehe rasmi ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa Wanachama.

Taarifa hiyo iliyotolewa leo Jumapili na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori, imebainisha kuwa tarehe rasmi ya Mkutano Mkuu huo itawekwa wazi mara baada ya kukamilika kwa kikao hicho cha Bodi.

Hatua hii imekuja kufuatia kusambaa kwa taarifa zilizoeleza kuwa Klabu ya Simba ilifanya Mkutano Mkuu wa dharura pamoja na dua maeneo ya Bunju, jijini Dar es Salaam, ambapo pia ilidaiwa kuwa Baraza Jipya la Wadhamini liliundwa. Taarifa hizo zilidai kuwa waliopitishwa kwenye baraza hilo ni Salim Abdallah Muhene, Dk. Bill Kiwia, Alhaj Ismail Mohamed, Amos Makala, Adam Mgoi, Hamad Abdallah pamoja na Hassan Hasanoo.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Mwenyekiti Magori amewataka wanachama na mashabiki kupuuzia maamuzi hayo kwani si halali.

Tunapenda kuwataarifu wanachama wote wa Simba kuwa hicho kilichofanyika Bunju siku ya leo siyo kikao rasmi cha Mkutano Maalum wa Simba. Hivyo maamuzi yote yaliyotangazwa huko ni batili na kinyume cha Katiba ya Simba,” ilifafanua taarifa hiyo.

Magori aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya Simba ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2026 (Ibara ya 23), Mkutano Mkuu Maalum huandaliwa na Mwenyekiti wa Klabu kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi.

“Hivyo kesho tarehe 3/8/2026 kutakuwa na kikao cha Bodi kujadili ajenda ya Mkutano Mkuu maalum wa Wanachama. Mtajulishwa siku maalum ya Mkutano huo,” ilihitimisha taarifa hiyo.

Hersi Said Afunguka Usajili wa Yanga 2026/27: “Bado Mchezaji Mmoja!”