Francis Baraza Pamba Jiji
Yanga SC

Baraza Afunguka Baada ya Kipigo cha Yanga: Aweka Wazi Tatizo la Pamba Jiji

Vardo August 29, 2026 10:19 am

Kocha Mkuu wa Pamba Jiji FC, Francis Baraza, amekiri kuwa kikosi chake kinakabiliwa na changamoto kubwa ya kutumia nafasi na ufungaji wa mabao, huku akiahidi kufanya marekebisho ya haraka baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Yanga SC.

Pamba Jiji ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam. Yanga ilitumia vyema makosa ya Pamba Jiji na kuondoka na pointi zote tatu.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mchezo huo, Baraza alisema licha ya wachezaji wake kuonyesha ushindani na jitihada kubwa, makosa machache yaliyojitokeza ndiyo yaliyowagharimu.

Ufungaji Unavyoisumbua Pamba Jiji

Kocha huyo raia wa Kenya alibainisha kuwa kutokutumia nafasi zinazotengenezwa imekuwa sumu kwa timu hiyo katika michezo ya hivi karibuni.

“Nimeona kwenye mchezo wa leo kuna makosa kidogo ambazo tutazifanyia kazi. Tunahitaji kupush zaidi ili tuweze kupata matokeo mazuri. Leo tumekosa bao, na huu ni mchezo wetu wa tatu tunashindwa kupata bao. Hili ni jambo ambalo tunapaswa kulifanyia kazi kwa haraka, tuangalie wapi tunakosea na turekebishe,” alisema Baraza.

Mpango wa Kurejesha Utulivu Kwenye Kikosi

Akiangazia suluhu ya tatizo hilo, Baraza amesisitiza umuhimu wa kusaidia wachezaji wake kisaikolojia ili kuondoa presha wanapokuwa ndani ya eneo la hatari la mpinzani.

“Tumepata nafasi ambazo tungeweza kuzitumia vizuri. Tunahitaji kuhakikisha vijana hawapati presha na wanakuwa na utulivu pamoja na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanapopata nafasi.”

Licha ya matokeo hayo mabaya, Baraza anaamini kikosi chake kitaonyesha mwitikio chanya katika mechi zinazofuata za Ligi Kuu.

“Najua kwenye mchezo unaokuja vijana wataonyesha kiwango kizuri zaidi. Kama kocha, nitaendelea kufanyia kazi haya mapungufu. Ni pole kwa kupoteza, lakini macho yetu yote yapo mbele,” alihitimisha Baraza.

Vita Ya Fainali CECAFA Women 2026: Kawempe Yaisaka CBE, Police Bullets Kuikabili Yei Manqoba Mngqithi Aweka Mipango Hadharani Yanga SC